Septemba 26,2022; Jumatatu: Juma La 26 La Mwaka

Wat. Kosma na Damiano, Mashahidi
Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Ayu. 1:6-22

Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao. Bwana akamwuliza, Shetani, “Umetoka wapi wewe?” Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, “Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.” Kisha Bwana akamwuliza Shetani, “Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na uelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.” Ndipo shetani akamjibu Bwana, na kusema, “Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukingo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibariki, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.” Bwana akamwambia shetani, “Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe.” Basi shetani akatoka mbele za uso wa Bwana. Ilitukia siku moja hao wanawe na binti zake walipokuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, mjumbe akamfikilia Ayubu na kumwambia, “Hao ng’ombe walikuwa wakilima, na punda walikuwa wakilisha karibu nao; mara Waseba wakawashambulia, wakawachukua wakaenda nao; naam wamewaua hao watumishi kwa makali ya upanga, mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.” Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, “Moto wa Mungu umeanguka kutoka mbinguni na kuwateketeza kondoo, na wale watumishi, na kuwaangamiza; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.” Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, “Wakaldayo walifanya vikosi vitatu, wakawaangukia ngamia, wakaenda nao, naam, wamewaua wale watushi kwa makali ya upanga; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.” Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, “Wanao na binti zako walikuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa; mara, tazama, upepo wenye nguvu ukatoka pande za jangwani, ukaipiga hiyo nyumba pembe zake nne, nayo ikawaangukia hao vijana, nao wamekufa; na mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.” Ndipo Ayubu akainuka, akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake, na kuanguka na nchi, na kusujudia; akasema, “Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko nili uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la bwana na libarikiwe.” Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 17:1-3, 6-7

 1. Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio change,
  Utege sikio lako kwa maombi yangu,
  Yasiyotoka katika midomo ya hila.

K: Utege sikio lako ulisikie neno langu.

 1. Hukumu yangu na itoke kwako,
  Macho yako na yatazame mambo ya adili.
  Umenijaribu moyo wangu, umenijilia usiku,
  Umenihakikisha usione neno. (K)
 2. Ee Mungu nimekuita kwa maana utaitika,
  Utege sikio lako ulisikie neno langu;
  Dhihirisha fadhili zako za ajabu,
  Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia. (K)

INJILI: Lk. 9:46-50

Wanafunzi walianza kuhojiana, ni nani atakayekuwa mkubwa miongoni mwao. Naye Yesu alipotambua mawazo ya mioyo yao, alitwaa mtoto mdogo akamweka karibu naye, akawaambia, “Yeyote atakayempokea mtoto huyu kwa jina langu anipokea mimi; na ye yote atakayenipokea mimi ampokea yeye aliyenituma. Kwa kuwa aliye mdogo miongoni mwenu nyote huyo ndiye mkubwa.” Yohane akajibu akamwambia, “Bwana mkubwa, tuliona mtu anatoa pepo kwa jina lako; tukamkataza, kwa sababu hafuatani na sisi; Yesu akamwambia, “Msimkataze, kwa kuwa yeye ambaye si kinyume chenu yu upande wenu.”

TAFAKARI
UKUBWA WA MBATIZWA NI UTUMISHI: Jana tuliusikia utabiri wa Yesu kuhusu mateso, kifo na ufufuko. Tukiyafuata mafundisho ya Yesu, mkubwa ni yule ambaye yupo tayari kwa utumishi, yule ajitoaye kwa ajili ya wengine. Yesu alionyesha hili kwa mfano hai alipojinyenyekeza na kutwaa hali ya utumishi (Phil 2:5). Unyenyekevu bila hila ndiyo ukubwa wa wabatizwa, hivyo tuige unyenyekevu wa watoto bila kujikweza. Tumesikia Yohane akijitangaza kwa Yesu kwa kumzuia mtu kufanya utume kwa jina la Yesu. Jambo hili halikuwa sifa kwa Yohane bali Yesu alianza kutoa Katekesi kwake na kwetu. Kwa Katekesi hii Yesu anatufundisha kuwa kundi fulani la Wakristo wasipinge utume au umisionari unaofanywa na kundi lingine kwa jina la Kristo. Ukubwa katika Ukristo upo katika kuwa Mkristo hivyo tusiwe sababu ya kuzuia kazi ya Mungu kutendeka. Utume wa Mkristo yeyote ulenge katika kumtangaza Kristo na siyo kujitangaza kwa masilahi binafsi. Tukumbuke kuwa Roho wa Mungu huvuma apendako na hivyo tusizuie kazi ya Mungu.

SALA: Ee Yesu, naomba roho ya utumishi na unyenyekevu.