Septemba 24,2022; Jumamosi: Juma La 25 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Mhu. 11: 9 – 12: 8

Wewe, kijana uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako; lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hukumuni. Kwa hiyo ondoa majonzi moyoni mwako, nawe uuondoe ubaya mwilini mwako; kwa maana ujana ni ubatili, na utu uzima pia. Mkumbuke Muumba wako, siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, wala haijakaribia miaka utakaposema, “Mimi sina furaha katika hiyo”. Kabla jua, na nuru, na mwezi, na nyota, havijatiwa giza; kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua; Siku ile walinzi wa nyumba watakapotetema; hapo wenye nguvu watakapojiinamisha; na wasagao kukoma kwa kuwa ni haba; na hao wachunguliao madirishani kutiwa giza; na milango kufungwa katika njia kuu; sauti ya kinu itakapokuwa ni ndogo; na mtu kusituka kwa sauti ya ndege; na binti za kuimba watapunguzwa; naam, wataogopa kilichoinuka; na vitisho vitakuwapo njiani; na mlozi utachanua maua; na panzi atakuwa ni mzigo mzito; na pilipili hoho itapasuka; maana mtu aiendea nyumba yake ya milele. Nao waombolezao wazunguka njiani. Kabla haijakatika kamba ya fedha; au kuvunjwa bakuli la dhahabu; au mtungi kuvunjika kisimani; au gurudumu kuvunjika birikani; nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa. Mhubiri asema, Ubatili mtupu; mambo yote ni ubatili!

Wimbo Wa Katikati: Zab. 90: 3-6, 12-14, 17

 1. Wamrudisha mtu mavumbini,
  Usemapo, Rudini, enyi wanadamu.
  Maana miaka elfu machoni pako
  Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
  Na kama kasha la usiku.

K: Wewe Bwana, umekuwa makao yetu,
kizazi baada ya kizazi.

 1. Wawagharikisha, huwa kama usingizi,
  Asubuhi huwa kama majani yameavyo.
  Asubuhi yachipuka na kumea,
  Jioni yakatika na kukauka. (K)
 2. Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu,
  Tujipatie moyo wa hekia.
  Ee Bwana, urudi, hata lini?
  Uwahurumie watumishi wako. (K)
 3. Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako,
  Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.
  Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu,
  Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti. (K)

INJILI: Lk. 9: 43-45

Makutano walipokuwa wakiyastaajabia mambo yote aliyoyafanya, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu.” Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile.

TAFAKARI
IMANI KWA YESU NA UDHIA HAVITENGANISHWI: Injili ya leo inalitangaza Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko. Wanafunzi wa Yesu hawakuelewa jambo hili kwani bado walikuwa na mtazamo wa kumpata masiha wa kidunia na siyo masiha wa msalaba. Yesu kutangaza kuwa atateswa msalabani haikuwa rahisi wafuasi wake kulipokea, lilikuwa fumbo. Hawakuweza kumwelewa masiha ambaye anaonekana kuwa mtumishi badala ya mfalme. Kitendo cha Yesu kuteseka msalabani na kumwaga damu yake kwa ajili yetu inaonyesha namna alivyotupenda. Hii inatupa maana ya mateso kwa Mkristo. Yesu anatufundisha maisha ya sadaka ya kujitoa kabisa kwa ajili ya kulinda na kutetea imani. Masharti ya kuwa mfuasi wa Yesu ni kujikana na kuchukua msalaba (mateso) kama ilivyokuwa kwake siku ya Ijumaa Kuu na tukaona matunda yake pasaka. Penye Msalaba panao utukufu. Tusiyakimbie mateso yasababishwayo na maisha ya ufuasi, bali tuyakabili kwa imani.

SALA: Ee Yesu, nijalie moyo wa kuvumilia mateso yasababishwayo na maisha ya ufuasi. Amina.