Septemba 23,2022; Ijumaa: Juma La 25 La Mwaka

Pio of Pietrelcina, p M
Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Mhu. 3:1-11

Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; wakati wa kupanda, na wakati wa kung’oa yaliyopandwa; wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga; wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza; wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia; wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa; wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena; wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; wakati wa vita, na wakati wa amani. Je! Mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo? Nimeiona taabu ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake. Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 144: 1-4

 1. Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu,
  Mhisani wangu na boma langu,
  Ngome yangu na Mwokozi wangu,
  Ngao yangu niliyemkimbilia.

K: Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu.

 1. Ee Bwana, mtu ni kitu gani hata umjue?
  Na binadamu hata umwangalie?
  Binadamu amefanana na ubatili,
  Siku zake ni kama kivuli kipitacho. (K)

INJILI: Lk. 9:18-22

Yesu alipokuwa akisali kwa faragha, wanafunzi wake walikuwapo pamoja naye, akawauliza, “Je! Makutano hao wanasema ya kuwa mimi ni nani?” Wakamjibu wakisema, “Yohane Mbatizaji; lakini wengine, Eliya; na wengine kwamba mmoja wapo wa manabii wa kale amefufuka.” Akawaambia, “Nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani?” Petro akamjibu akasema, “Ndiwe Kristo wa Mungu”. Akawaonya, akawakataza wasimwambie mtu neno hilo. Akisema, “Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka.”

TAFAKARI
KUMTAMBUA YESU KATIKA MAISHA YA KILA SIKU: Katika Injili ya leo tumemsikia Yesu akitaka mrejesho kutoka kwa wafuasi wake. Baada ya kukaa nao na kuwafundisha anataka kupata tathimini kama ameeleweka au la. Majibu yaliyotolewa kuhusu Yesu ni nani, yalitofautiana kutokana na uelewa wao. Hii inaonyesha kuwa Wakristo wote tunamwamini Kristo ingawa kuna wanaomwelewa kwa njia tofauti tofauti. Majibu yaliyotolewa kuwa Yesu ni Yohane, Eliya au Nabii wa Kale aliyefufuka hayakutosheleza kumweleza Yesu ni nani. Kwa neema ya Mungu Petro anatambua kuwa ndiye Masiya alyekuwa anasubiriwa na watu na hivyo amekuja kukamilisha ahadi. Swali ambalo Yesu amewauliza mitume sisi nasi tunaulizwa swali hilohilo. Tujiulize tunampa Yesu nafasi gani katika maisha yetu. Baada ya Petro kutoa jibu ni vizuri pia kujiuliza kama tunatoa jibu linalofanana kumhusu Yesu. Kama kuna makandokando yanayotuzuia kumfahamu Yesu, sasa ni muda wa kuyaondoa ili niweze kumshuhudia kwa maisha yangu.

SALA: Ee Yesu, nifanye nitambue nafasi yako katika maisha yangu. Amina.