Septemba 22,2022; Alhamisi: Juma La 25 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Mhu. 1:2-11

Mhubiri asema, “Ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili. Mtu ana faida gani ya kazi yake yote aifanyayo chini ya jua? Kizazi huenda, kizazi huja; naye dunia hudumu daima. Jua lachomoza, na jua lashuka, na kufanya haraka kwenda mahali pa mawio yake. Upepo huvuma kusi, hugeuka kuwa kaskazi; hugeuka daima katika mwendo wake, na upepo huyarudia mazunguko yake. Mito yote huingia baharini, walakini bahari haijai; huko iendako mito, ndiko irudiko tena. Mambo yote yamejaa uchovu usioneneka, jicho halishibi kuona, wala sikio halikinai kusikia. Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako; na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka; wala jambo jipya hakuna chini ya jua. Je! kuna jambo lo lote ambalo watu husema juu yake, tazama, ni jambo jipya? Limekwisha kuwako, tangu zamani za kale zilizokuwa kabla yetu sisi. Hakuna kumbukumbu lo lote la vizazi vilivyotangulia; wala hakutakuwa na kumbukumbu lo lote la vizazi vitakavyokuja, miongoni mwao wale watakaofuata baadaye.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 90:3-6, 12-14, 17

 1. Warudisha mtu mavumbini,
  Usemapo, rudini enyi wanadamu.
  Maana miaka elfu machoni pako
  Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
  Na kama kasha la usiku.

K: Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu,
kizazi baada ya kizazi.

 1. Wawagharikisha huwa kama usingizi,
  Asubuhi huwa kama majani yameayo.
  Asubuhi yachipuka na kumea,
  Jioni yakatika na kukauka. (K)
 2. Basi, utujulishe kuzihesabu siku siku zetu,
  Tujipatie moyo wa hekima.
  Ee Bwana, urudi, hata lini?
  Uwahurumie watumishi wako. (K)
 3. Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako,
  Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.
  Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu,
  Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti. (K)

INJILI: Lk. 9:7-9

Herode mfalme alisikia habari za yote yaliyotendeka, akafadhaika kwa sababu watu wengine walisema ya kwamba Yohane amefufuka katika wafu, na wengine ya kwamba Eliya ametokea, na wengine ya kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka. Lakini Herode akasema, “Yohane niliyemkata kichwa; basi ni nani huyu ambaye ninasikia mambo haya juu yake?” Akataka kumwona.

TAFAKARI
TUMTAFUTE YESU KWA NIA NJEMA: Katika Injili ya leo tumewasikia watu wakijaribu kumtambua Yesu kwa kuanzia na watu waliowafahamu. Namna walivyomtambua Yesu kwa picha ya Agano la Kale waliyokuwanayo haikuwa sahihi kwani Yesu ni mkuu zaidi. Yawezekana kwa kuwa Herode alishamwua Yohane, sasa anataka kumwua Yesu ambaye Yohane alikuwa akitangaza habari zake. Cha kushangaza ni kuwa Yesu haogopi hila za Herodi kwani hata alipoambiwa anataka kumwua alijibu, “Nendeni mkamwambie huyo mbweha leo na kesho ninafukuza mapepo na kuponya wagonjwa na siku ya tatu nitakamilisha kazi yangu” (Lk 13:32). Saa ya mateso ilipofika Pilato alimtoa Yesu ahukumiwe na Herode ila Yesu hakumjibu chochote kwani hakustahili kujibiwa. Tumtafute Yesu kwa lengo la kuimarika zaidi kiroho. Leo hii katika taifa letu wapo watu wanaomtafuta Yesu siyo kwa lengo la kukutana na Mungu bali kwa malengo kama kukutana na utajiri wa haraka, kuimarika kiuchumi na kiafya. Lengo letu la kukutana na Yesu lisukumwe zaidi na lengo la kimbingu.

SALA: Ee Yesu, naomba unijalie nia njema ya ufuasi. Amina.