Septemba 20,2022; Jumanne: Juma La 25 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Mit. 21:1-6, 10-13

Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa Bwana; kama mfereji wa maji huugeuza po pote apendapo. Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe; bali Bwana huipima mioyo. Kutenda haki na hukumu humpendeza Bwana kuliko kutoa sadaka. Macho yenye kiburi, na moyo wa kutakabari, hata ukulima wa waovu, ni dhambi. Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu; bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji. Kupata akiba ya mali kwa ulimi wa uongo ni moshi upeperushwao; ni kutafuta mauti. Nafsi ya mtu mbaya hutamani maovu; jirani yake hapati fadhili machoni pake. Mwenye mzaha aadhibiwapo, mjinga hupata hekima; na mwenye hekima afundishwapo, hupokea maarifa. Mwenye haki huitafakari nyumba ya mtu mbaya; jinsi wabaya waangushwavyo wakaangamia. Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini, yeye naye atalia, lakini hatasikiwa.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 119:27, 30, 34-350

  1. Heri wali kamili njia zao,
    Waendao katika sharia ya Bwana.
    Unifahamishe njia ya mausia yako,
    Nami nitayatafakari maajabu yako.

K: “Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako,
Ee Bwana.”

  1. Nimeichagua njia ya uaminifu,
    Na kuziweka hukumu zao mbele yangu.
    Unifahamishe nami nitaishika sheria yako,
    Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote. (K)
  2. Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako,
    Kwa maana nimependezwa nayo.
    Nami nitaitii sheria yako daima,
    Naam, milele na milele. (K)

INJILI: Lk. 8:19-21

Walimwendea Yesu mama yake na ndugu zake, wasiweze kumkaribia kwa sababu ya mkutano. Akaletewa habari akiambiwa, “Mama yako na ndugu zako wamesimama nje wakitaka kuonana nawe.” Akawajibu akasema, “Mama yangu na ndugu zangu ndio hao walisikao neno la Mungu na kulifanya.”

TAFAKARI
SISI NI NDUGU ZAKE YESU KRISTO: Katika Injili Yesu anatuhakikishia kuwa wote wanaosikia Neno la Mungu na kulishika ni ndugu zake. Kwa ubatizo wetu sisi ni ndugu za Yesu Kristo. Yesu anapopata ujumbe kuwa ndugu zake, na mama yake wanamtafuta, aliongeza ukubwa wa familia yake kwa kuwajumuisha wote watekelezao neno lake. Yesu hakubali familia yake imtoe katika utume wake. Neno la Mungu linatengeneza familia mpya katika Kristo. Kwa wale waliokubali kumpokea Kristo aliwapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu. Sote tunaalikwa kuwa sehemu ya hii familia mpya ya Yesu Kristo. Tuwaombee viongozi wetu wa kiroho, ambao kwa Sakramenti ya Daraja wamekuwa na familia mpya waweze kujitoa zaidi kuhudumia familia hiyo. Wasijitokeze wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki watakaojaribu kuwatoa viongozi hawa katika utume wao. Wakifanya hivyo watashindwa kujumuika katika familia mpya ya Kristo.

SALA: Ee Yesu, naomba unijalie uaminifu katika familia mpya ya Kikristo.Amina.