Septemba 19,2022; Jumatatu: Juma La 25 La Mwaka

Mt. Januari, Askofu na Shahidi
Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Mit. 3:27-34

Mwanangu, Usiwanyime watu mema yaliyo haki yao, ikiwa katika uwezo wa mkono wako kuyatenda. Usimwambie jirani yako, “Nenda, urudi halafu, na kesho nitakupa,” nawe unacho kitu kile karibu nawe. Usiwaze mabaya juu ya jirani yako, ambaye anakaa karibu nawe na kujiona salama. Usishindane na mtu bila sababu, ikiwa hakukudhuru kwa lo lote. Usimhusudu mtu mwenye jeuri, wala usiichague mojawapo ya njia zake. Maana mtu mkaidi ni chukizo kwa Bwana, bali siri yake ni pamoja na wanyofu. Laana ya Bwana i katika nyumba ya waovu, bali huibariki maskani ya wenye haki. Hakika yake huwadharau wenye dharau, bali huwapa wanyenyekevu neema.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 15

 1. Ni nani atakayefanya maskani yake
  Katika kilima chako kitakatifu.
  Ni mtu aendaye kwa ukamilifu,
  Na kutenda haki, asemaye kweli kwa moyo wake
  Asiyesingizia kwa ulimi wake.

(K) Mtu aendaye kwa ukamilifu, atafanya maskani yake,
katika kilima chako kitakatifu.

 1. Asiyemtendea mwenziwe mabaya,
  Wala hakumsengenya jirani yake.
  Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa,
  Bali huwaheshimu wamchao Bwana.
  Ingawa ameapa kwa hasira yake,
  Hayabadili maneno yake. (K)
 2. Hakutoa fedha yake apate kula riba,
  Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia.
  Mtu atendaye mambo hayo
  Hataondoshwa milele. (K)

INJILI: Lk. 8:16-18

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Hakuna mtu ambaye akiisha washa taa huifunika kwa chombo, au kuiweka uvunguni, bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuona nuru yake. Kwa maana hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa ambalo halitajulikana na kutokea wazi. Jiangalieni basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang’anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho.”

TAFAKARI
MATENDO MEMA NI MWANGA KWA WENGINE: Leo Yesu anaendelea kufundisha kwa mifano, na anatumia mfano wa taa. Sote tunafahamu umuhimu wa taa na mahali pa kuiweka ili tunufaike na mwanga wake. Ikiwekwa mahali pasipostahili mwanga hautatufikia na hatutaona matunda ya mwanga wake. Neno la Mungu ni taa ya kutuondoa katika giza. Tusipofungua Biblia zetu na kusoma Neno la Mungu tunazidi kubaki katika giza. Tukiwa na Biblia bila kuisoma ni sawa na taa iliyowashwa na kuwekwa uvunguni au kufunikwa. Neno hilo likiwekwa mezani na kusomwa linaangaza maisha ya wote wanaoishi kwenye nyumba. Kwa mfano huu, Yesu anatueleza kuwa sisi kama Wakristo hatupaswi kuogopa kuwa mashahidi wa Habari Njema na watangazaji wake. Vinywa vyetu wakati wa ubatizo vilifumbuliwa kwa kuambiwa “efata” ili tutangaze makuu ya Mungu. Tusiogope kuwa watangazaji wa Neno la Mungu kwa watu wote.

SALA: Ee Mungu, naomba unijalie ujasiri wa kutangaza makuu yako.Amina.