Septemba 18,2022; Jumapili: Jumapili Ya 25 Ya Mwaka

MWAKA C
Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Amo. 8:4-7

Lisikieni hili, ninyi mnaopenda kuwameza wahitaji, na kuwakomesha maskini wa nchi, mkisema, “Mwezi mpya utaondoka lini, tupate kuuza nafaka? Na sabato nayo, tupate kuandika ngano? Mkiipunguza efa na kuiongeza shekeli, mkidanganya watu kwa mizani ya udanganyifu, tupate kuwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu; na kuziuza takataka za ngano. Bwana ameapa kwa fahari ya Yakobo, Hakika sitazisahau kamwe kazi zao hata mojawapo.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 113:1-2, 4-8

 1. Aleluya.
  Enyi watumishi wa Bwana, sifuni,
  Lisifuni jina la Bwana;
  Jina la Bwana lihimidiwe,
  Tangu leo na hata milele.

K: Msifuni Bwana anayewakweza maskini.

 1. Bwana ni Mkuu juu ya mataifa yote,
  Na utukufu wake ni juu ya mbingu.
  Ni nani aliye mfano wa Bwana,
  Mungu wetu aketiye juu;
  Anyenyekeaye kutazama, mbinguni na duniani? (K)
 2. Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
  Na kumpandisha maskini kutoka jaani.
  Amketishe pamoja na wakuu,
  Pamoja na wakuu wa watu wake. (K)

SOMO 2: 1 Tim. 2:1-8

Kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu. Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli. Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake. Nami kwa ajili ya huo naliwekwa niwe mhubiri na mtume, (nasema kweli, sisemi uongo), mwalimu wa Mataifa katika imani ya kweli. Basi, nataka wanaume wasalishe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano.

SHANGILIO 1Sam 3:9; Yn. 6:68

Aleluya, aleluya,
Nena Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia;
Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.

INJILI: Lk. 16:1-13

Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyekuwa na wakili wake; huyu alishitakiwa kwake kuwa anatapanya mali zake.” Akamwita, akamwambia, “Ni habari gani hii ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili tena.” Yule wakili akasema moyoni mwake, “Nifanyeje? Maana, bwana wangu ananiondolea uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya. Najua nitakalotenda, ili nitakapotolewa katika uwakili, wanikaribishe nyumbani mwao.” Akawaita wadeni wa bwana wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza, “Wawiwani na bwana wangu?” Akasema, “Vipimo mia vya mafuta.” Akamwambia, “Twaa hati yako, keti upesi, andika hamsini.” Kisha akamwambia mwingine, “Na wewe wawiwani?” Akasema, “Makanda mia ya ngano.” Akamwambia, “Twaa hati yako, andika themanini.” Yule bwana akamsifu wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru.

Nami nawaambia, “Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu, ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele.

Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia. Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli? Na kama hamkuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe? Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu na kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.”

TAFAKARI
MALI IWE NYENZO YA WOKOVU NA SIYO ENZI: Wazo hili linatafsirika kutoka Injili tuliyosomewa na linaungwa mkono na masomo yanayoisindikiza. Injili inasimulia jinsi wakili asiye mwaminifu alivyocheza karata vizuri na mali ya dunia kusudi aishi vizuri baada ya kufukuzwa kazi. Mfano huu umejikita katika mazingira ya ufukara wa Israeli. Kutokana na uhaba wa ardhi na uchache wa mvua Israeli ilikuwa na uchumi duni. Ajira zilikuwa haba na ufukara ulikuwa si jambo la kushangaza. Shughuli za uchumi hazikuwa zenye kuwaletea watu ukwasi mkubwa sana. Baadhi ya watu walikuwa wakulima, wengine wafugaji, wengine wavuvi na wengine watu waliojishughulisha na viwanda vidogo vidogo, kama vile, utengenezaji wa nguo kwa manyoya ya kondoo, utengenezaji wa vifaa vya ngozi, ufinyanzi, uhunzi, ujenzi na useremala. Hivi katika mazingira hayo kupata uwakili ilikuwa fursa ya kupendeza sana. Ndipo yule wakili alipofahamishwa kwamba atafukuzwa kazi kutokana na kutofanya kazi yake vizuri alipata hofu kubwa maana kupata kazi nzuri kama ile ilikuwa ni bahati nasibu. Lakini basi akagundua jambo la kutenda kusudi atakapotolewa katika uwakili, watu wamkaribishe majumbani mwao. Ndipo alipowaita wadeni wa bwana wake, kila mmoja na kuwapunguzia madeni yao.
Ujanja huu wa kujinusuru wakati wa mwambo ndiyo anaotaka Yesu tuutafakari mintarafu mwisho wetu kihistoria. Tukiaga dunia, je tutakaribishwaje mbinguni? Tunachezaje karata ya mustakabali mwema wa kiroho ili tuweze kuingia mbinguni? Kifupi anatutaka tutumie kila nyenzo kusudi tukubalike mbinguni.
Somo la kwanza linawatahadharisha watu wote wanaopenda kudhulumu vitu na watu. Ni somo linaloangazia mustakabali mbaya wa wadhalimu, wale wanaopenda kuwameza wahitaji, na kuwakomesha maskini wa nchi, wakiulizana kwa uroho, lini utakapoonekana mwezi mpya wapate kuuza nafaka na lini itafika sabato wapate kuandika ngano. Pamoja nao ni wale wanaopenda kupunja vipimo, kwa mfano, kuipunguza efa na kuiongeza shekeli, wakidanganya watu kwa mizani za udanganyifu. Aidha ni wale wanaoulizia mwezi utakapoandama wapate kuwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu pamoja na kuziuza takataka za ngano. Mwishoni somo linakomelea mambo kwa kueleza jinsi Bwana alivyoapa kwamba hatazisahau kamwe kazi za waovu hawa hata mojawapo. Hii ina maana kuwa Mungu atawaadhibu wote wanaotenda dhambi bila kutubu.
Somo la pili linapendekeza tuombeane kusudi watu wote, yaani hata wenye vyeo vya juu sana, yaani pamoja na wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu. Ni kwa sababu Mungu hataki yeyote apotee bali anataka watu wote waokolewe. Tena ni kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote. Mwishoni mtume Paulo anaeleza nafasi yake akisema amewekwa awe mhubiri, mtume na mwalimu wa Mataifa katika imani ya kweli. Tukijumlisha tunaaswa leo tutumie kila tulichonacho, mali, karama, vyeo na kadhalika kama nyenzo za wokovu na siyo sababu za kulimatia kwenye enzi. Haya tumakinike sote.

SALA: Ee Mungu mwema, tunakuomba utufundishe siku zote namna ya kutumia pesa, mali, karama na vitu vizuri vyote tulivyonavyo kama nyenzo za kukufikia wewe mwishoni mwa maisha haya. Amina.