Septemba 16,2022; Ijumaa: Juma La 24 La Mwaka

Wat. Korneli, Baba Mt. na Sipriano Askofu, Mashahidi
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: 1 Kor. 15: 12-20

Ikiwa Kristo anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu, mbona baadhi yenu husema kwamba hakuna kiyama ya wafu? Lakini kama hakuna kiyama ya wafu, Kristo naye hakufufuka; tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yetu ni bure. Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi. Maana kama wafu hawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu. Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea. Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote. Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 17: 1, 6-8, 15

 1. Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu,
  Utege sikio lako kwa maombi yangu
  Yasiyotoka katika midomo ya hila.

K: Nishibishwe, Ee Bwana, kwa sura yako.

 1. Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika,
  Utege sikio lako ulisikie neno langu.
  Dhihirisha fadhili zako za ajabu,
  Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia;
  Kwa mkono wako wa kuume
  Uwaokoe nao wanaowaondokea. (K)
 2. Unilinde kama mboni ya jicho lako,
  Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako;
  Bali mimi nikutazame uso wako katika haki,
  Niamkapo nishibishwe kwa sura yako. (K)

INJILI: Lk. 8: 1-3

Yesu alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, na Yohana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.

TAFAKARI
NAFASI YA MWANAMKE KUMTANGAZA KRISTO: Katika Injili ya leo tunapata mwendelezo wa Injili ya jana ambapo Yesu anaendelea kuwa na mtazamo tofauti wa wakati wake kuhusu wanawake. Leo katika Injili Yesu yupo na mitume pamoja na wafuasi wanawake jambo ambalo si la kawaida kwa utamaduni wa wakati ule. Mwinjili Luka anawaweka mitume na wafuasi wanawake katika ngazi moja kwa sababu wote wanamfuata Yesu. Jambo hili ni kielelezo kuwa Yesu anafanya kazi na watu wote. Katika Kanisa na nje ya kanisa wakati fulani wanaharakati wa kutafuta usawa wamejaribu sana kuhamasisha wanawake wapewe sakramenti ya daraja kama wanaume. Ukweli ni kuwa kumtumikia Mungu siyo kwa njia ya upadre tu. Kina mama wanazo nafasi nyingi za kumtumikia Yesu ikiwa ni pamoja na maisha ya ufuasi. Yesu amepokea majitoleo yao ya ufuasi. Kina mama wanaalikwa kuendelea kuwa wafuasi wa Kristo kila siku kwa utumishi wao.

SALA: Ee Yesu, nijalie moyo wa kuwaheshimu kina mama wote.Amina.