Septemba 15,2022; Alhamisi: Juma La 24 La Mwaka

Bikira Maria Mt. wa Mateso
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: 1Kor. 15:1-11

Ndugu zangu, nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri; isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara; baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala; baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote; na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake. Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu naliliudhi kanisa la Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami. Basi, kama ni mimi, kama ni wale, ndivyo tuhubirivyo, na ndivyo mlivyoamini.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 118: 1-2, 15-17 28

  1. Aleluya.
    Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
    Kwa maana fadhili zake ni za milele.
    Israeli na aseme sasa,
    Ya kwamba fadhili zake ni za milele.

K: Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.

  1. Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa;
    Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
    Sitakufa bali nitaishi,
    Nami nitayasimulia matendo ya Bwana. (K)
  2. Ndiwe Mungu wangu, nami nitakushukuru,
    Ndiwe Mungu wangu, name nitakutukuza. (K)

INJILI: Lk. 7:36-50

Mtu mmoja katika Mafarisayo alimwalika Yesu ale chakula kwake; akaingia katika nyumba yake yule Farisayo, akaketi chakulani. Na tazama, mwanamke mmoja wa mji ule, aliyekuwa mwenye dhambi, alipopata habari ya kuwa ameketi chakulani katika nyumba ya yule Farisayo, alileta chupa ya marimari yenye marhamu. Akasimama nyuma karibu na miguu yake, akilia, akaanza kumdondoshea machozi yake, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake, akiibusu-busu miguu yake na kuipaka yale marhamu. Basi, yule Farisayo aliyemwalika alipoona vile, alisema moyoni mwake, “Mtu huyu kama angekuwa nabii, angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi.” Yesu akajibu akamwambia, “Simoni, nina neno nitakalo kukuambia”. Akasema, “Mwalimu, nena.” Akasema, “Mtu mmoja mkopeshaji alikuwa na wadeni wawili; mmoja amwia dinari mia tano, na wa pili hamsini.” Nao walipokuwa hawana cha kumlipa, aliwasamehe wote wawili. Katika hao wawili ni yupi atakayempenda zaidi? Simoni akajibu akasema, “Nadhani ni yule ambaye alimsamehe nyingi.” Akamwambia, “Umeamua haki.” Akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, “Wamwona mwanamke huyu? Niliingia nyumbani kwako, hukunipa maji kwa miguu yangu; bali huyu amenidondoshea machozi miguu yangu; na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake. Wewe hukunibusu; lakini huyu tangu nilipoingia hakuacha kunibusu sana miguu yangu. Hukunipaka kichwa changu mafuta; bali huyu amenipaka miguu yangu marhamu.” Kwa ajili ya hayo nakuambia, “Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo.” Kisha alimwambia mwanamke, “Umesamehewa dhambi zako.” Ndipo wale walioketi chakulani pamoja naye walianza kusema mioyoni mwao, Ni nani huyu hata asamehe dhambi? Akamwambia yule mwanamke, “Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani.”

TAFAKARI
HURUMA YA MUNGU NI KWA WATU WOTE: Tumesikia katika Injili Yesu yupo nyumbani kwa Simoni. Alipokuwa chukulani anajitokeza mtu ambaye kwa tamaduni za wakati huo hakupaswa kupokelewa na Yesu, kwa sababu ni miongoni mwa wale waliotazamwa kama wadhambi. Yesu anaenda kinyume na utamaduni huu ambao si mzuri na anampokea kama watu wengine. Wafarisayo wanampinga Yesu kwa kukubali kwake kumpokea mama huyu mdhambi. Yesu anajibu pingamizi hili kwa kutumia mfano wa wadeni wawili waliosamehewa madeni yao. Mfano huu unaonyesha kuwa wote yaani mwanamke na Mfarisayo walisamehewa madeni yao na Yesu Kristo. Mfarisayo huyu alipokea upendeleo wa Yesu kwa kumwalika nyumbani kupata chakula na mwanamke huyu alionyesha shukrani kwa machozi yaliyoosha miguu ya Yesu na kuibusu na kuyapaka marashi. Mt. Ambrosi alisema katika kupata wokovu kuna maji na machozi. Maji kwa ajili ya ubatizo na machozi kwa ajili ya toba. Mama huyu ameonyesha kuwa wanaofanya toba ya kweli husamehewa dhambi zao.

SALA: Ee Yesu, nijalie moyo wa huruma kwa watu wote.