Septemba 13,2022; Jumanne: Juma La 24 La Mwaka

Mt. Yohane Krisostomi, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Kumbukumbu
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: 1Kor. 12:12-14, 27-31

Kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinywesha Roho mmoja. Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi. Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake. Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha. Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri? Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 100

  1. Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote;
    Mtumikieni Bwana kwa furaha;
    Njoni mbele zake kwa kuimba.

K: Tu watu wake na kondoo wa malisho yake.

  1. Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
    Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
    Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.
  2. Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru;
    Nyuani mwake kwa kusifu;
    Mshukuruni, lihimidini jina lake. (K)
  3. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
    Rehema zake ni za milele;
    Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)

INJILI: Lk. 7:11-17

Yesu alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, “Usilie.” Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, “Kijana, nakuambia, Inuka.” Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, “Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake.” Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kando kando.

TAFAKARI
UHAI UNA THAMANI KUBWA: Katika Injili tumesikia Yesu alivyomfufua mtoto wa mjane mmoja. Kabla ya tendo hili Yesu alionyesha huruma kubwa kwa huyu mama aliyekuwa amefiwa na mtoto wake. Yesu alivaa kwanza hali ya yule mama akaonja huzuni ya yule mama ndiyo maana alimhurumia. Mtakatifu Paulo anatuambia lieni pamoja na wanaolia. Kwa tendo hili Yesu anatuonesha kuwa nguvu ya uhai ni kubwa kuliko nguvu ya kifo. Tendo hili la kurudisha tena uhai linatufanya tutambue zaidi uwepo wa Yesu katika Maisha yetu ya kila siku katika shida na katika raha. Tunaalikwa kupeana moyo sisi kwa sisi tunapokumbana na magumu katika maisha kama maradhi, misiba na majanga, tushiriki katika mambo haya ya kijamii kwani Yesu aliyashiriki wa kwanza kabisa. Tunapokumbana na magumu ya maisha tusikate tamaa, tumkimbilie yeye kwani kila mara anatuambia inuka. Hata katika uchumi uliozorota bado Yesu anatuambia inuka tusiendelee kubaki katika hali hiyo.

SALA: Ee Bwana, naomba unijalie moyo wa kulinda na kutetea uhai. Amina.