Septemba 12,2022 Jumatatu: Juma La 24 La Mwaka

Mwaka 2
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: 1Kor. 11:17-26, 33

Katika kuagiza haya, siwasifu, ya kwamba mnakusanyika, si kwa faida bali kwa hasara. Kwa maana kwanza mkutanikapo kanisani nasikia kuna faraka kwenu; nami nusu nasadiki; kwa maana lazima kuwapo na uzushi kwenu, ili waliokubaliwa wawe dhahiri kwenu. Basi mkutanikapo pamoja haiwezekani kula chakula cha Bwana; kwa maana kila mmoja hutangulia kutwaa chakula chake katika kule kula; hata huyu ana njaa, na huyu amelewa. Je! Hamna nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu? Niwaambieni? Niwasifu? La! Siwasifu kwa ajili ya hayo. Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywa kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo. Kwa hiyo, ndugu zangu, mkutanikapo mpate kula, mngojane.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 40:6-8, 16

 1. Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
  Masikio yangu umeyazibua,
  Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
  Ndipo niliposema, Tazama nimekuja.

(K) Mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.

 1. Katika gombo la chuo nimeandikiwa,
  Kuyafanya mapenzi yako,
  Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu
  Naama, sheria yako ime moyoni mwangu. (K)
 2. Nimehubiri habari za haki katika kuanyiko kubwa,
  Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua. (K)
 3. Washangilie, wakafurahie,
  Wote wakutafutao.
  Waupendao wokovu wako
  Waseme daima, Atukuzwe Bwana. (K)

INJILI: Lk. 7:1-10

Yesu alipokwisha kuyamaliza maneno yake yote masikioni kwa watu, aliingia Kapernaumu. Na mtumwa wake akida mmoja alikuwa hawezi, karibu na kufa; naye ni mtu aliyempenda sana. Aliposikia habari za Yesu, alituma wazee wa Wayahudi kwake kumwomba aje amponye mtumwa wake. Nao walipofika kwa Yesu, walimsihi sana wakisema, “Amestahili huyu umtendee neno hili; maana, analipenda taifa letu, naye alitujengea sinagogi.” Basi Yesu akaenda pamoja nao.”

Hata alipokuwa si mbali na nyumba yake, yule akida alituma rafiki kwake, akamwambia, “Bwana, usijisumbue, maana mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; kwa hiyo nilijiona sistahili mwenyewe kuja kwako; lakini, sema neno tu, na mtumwa wangu atapona. Kwa maana mimi ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ huenda; na huyu, ‘Njoo,’ huja; na mtumwa wangu, ‘Fanya hivi,’ hufanya.”

Yesu aliposikia hayo alimstaajabia, akaugeukia mkutano uliokuwa ukimfuata, akasema, “Nawaambia, hata katika Israeli sijaona imani kubwa namna hii. Na wale waliotumwa waliporudi nyumbani, wakamkuta yule mtumwa ni mzima.”

TAFAKARI
IMANI KWA YESU KRISTO: Katika Injili ya leo, tumesikia Imani kubwa aliyonayo Akida mmoja. Imani yake ilimfanya ajione hana mastahili ya kumkaribisha Yesu nyumbani kwake. Akida huyu anatufundisha umuhimu wa kumwamini Mungu kwa moyo wote na kwa unyenyekevu mkubwa. Huyu alikuwa na fadhila za imani na unyenyekevu ndiyo maana uponyaji ulifanyika. Mfano huu unatuonyesha pia kuwa Yesu ni kimbilio letu wakati wote na katika hali zote. Imani aliyokuwa nayo Akida tuliyemsikia ni kubwa sana kwani aliamini kuwa bila uwepo wa Yesu hamna Maisha. Akida huyu anamwomba Yesu aseme neno tu. Hapa anaonekana kuwa na mabadiliko makubwa sana kiimani kwani Yesu alivyokuwa anatembea kumwelekea naye alikuwa anasafiri kuelekea kilele cha imani yake na kuwa kiumbe kipya. Alimkaribisha kwanza Yesu, kisha akakaribisha Neno la Yesu. Tunafundishwa kuwa Neno la Mungu linaponya, linaokoa, lina nguvu ajabu na lina uwezo mkubwa wa kutenda linapotumiwa sawasawa. Tupende neno la Mungu, tulisome tulielewe na tuliishi na kuliweka katika Maisha yetu.

SALA: Ee Yesu, naomba uniimarishe zaidi katika Imani. Amina.