Septemba 11,2022; Jumapili: Jumapili Ya 24 Ya Mwaka

MWAKA C
Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Kut. 32:7-11, 13-14

Bwana alimwambia Musa, “Haya! Shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao, wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha, wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, ‘Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokuwa katika nchi ya Misri.’” Tena Bwana akamwambia Musa, “Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu; basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize; nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu.”

Musa akamsihi sana Bwana, Mungu wake, na kusema, “Bwana, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu? Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu, nao watairithi milele.” Na Bwana akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 51:1-2, 10-11 15,17

 1. Ee Mungu, unirehemu,
  Sawasawa na fadhili zako.
  Kiasi cha wingi wa rehema zako,
  Uyafute makosa yangu.
  Unioshe kabisa na uovu wangu,
  Na dhambi yangu i mbele yangu daima.

(K) Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu.

 1. Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
  Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
  Usinitenge na uso wako,
  Wala roho takatifu usiniondolee. (K)
 2. Ee Bwana, uifumbue midomo wangu,
  Na kinywa changu kitazinena sifa zako.
  Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika,
  Moyo uliovunjika na kupondeka,
  Ee Mungu, utaudharau. (K)

SOMO 2: 1 Tim. 1:12-17

Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake; ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri; lakini nalipata rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani. Na neema ya Bwana wetu ilizidi sana, pamoja na imani na pendo lililo katika Kristo Yesu. Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi. Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote, niwe kielezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele. Sasa kwa Mfalme wa milele, asiyeweza kuona uharibifu, asiyeonekana, Mungu peke yake, na iwe heshima na utukufu milele na milele. Amina.

SHANGILIO Yn. 14:6

Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi Njia, na Ukweli na Uzima, asema Bwana;
Mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya.

INJILI: Lk. 15:1-31

(somo fupi)

Watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia Yesu wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung’unika, wakisema, “Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao.” Akawaambia mfano huu, akisema, “Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aenda akamtafute yule aliyepotea hata amwone? Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi.” Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, “Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea.” Nawaambia: Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu.

“Au kuna mwanamke gani mwenye shilingi kumi, akipotewa na moja, asiyewasha taa na kufagia nyumba, na kutafuta kwa bidii hata aione? Na akiisha kuiona, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimeipata tena shilingi ile iliyonipotea.’ Nawaambia: Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye.”

TAFAKARI
TULIPOTEA, MUNGU ANAINGIA GHARAMA KUTUTAFUTA: Wazo hili linasomeka wazi wazi kwenye Injili na linaungwa mkono na masomo mawili yanayoisindikiza. Yesu anatoa maneno ya faraja sana kwa watu ambao jamii ya Kiyahudi ilishawabagua kama watu waendao motoni. Yesu aliikuta jamii ya Kiyahudi imeshajigawanya katika makundi mawili: kundi la waendao mbinguni na kundi la waendao motoni. Katika kundi la waendao mbinguni walijiweka Mafarisayo, waandishi wa Sheria, Waeseni, Maherodi, makuhani pamoja na wakuu wao. Katika kundi la waendao motoni waliwekwa watozaushuru, wachungaji, washona viatu na makahaba. Hawa ndio wanaoitwa wadhambi katika Injili.
Mgawanyo huu ulifanywa kwa msingi mmoja, ndiyo kuwa na muda na torati. Mafarisayo walisema, watu wakiwa na muda na torati, watajua Mungu anataka nini, na watu wakijua Mungu anataka nini watafanya, na watu wakifanya anachotaka Mungu watampendeza, na watu wakimpendeza Mungu hatakuwa na lingine la kuwafanyia bali kuwaingiza mbinguni. Hawatampendeza na watu wasiompendeza hawatakuwa na lingine ila kuwatupa motoni.
Watu wa makundi hayo hawakutazamiwa kushirikiana. Wadhambi ilikuwa waachwe peke yao mwishoni wakione vizuri cha mtema kuni kilichomtoa kanga manyoya. Yesu alipofika duniani na Mafarisayo kumsikiliza walimtia katika kundi la waendao mbinguni. Lakini punde wakashangazwa naye kwa vile alivyoshirikiana na wadhambi wakati yeye alikuwa mtu wa kundi lao. Watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia Yesu wamsikilize lakini Mafarisayo na waandishi wakanung’unikia kawaida yake ya kuwakaribisha wenye dhambi na kula nao.
Yesu alisahihisha mawazo yao ya kikatili kwa mifano miwili tuliyosikia. Kwake Kristo hao wadhambi ni sawa na kondoo aliyepotea kati ya kondoo mia moja ambaye lazima atafutwe kwa bidii yote naye akipatikana awe sababu ya furaha kubwa. Mfano wa pili wanalingana na shilingi iliyopotea kati ya kumi ambayo lazima itafutwe kwa jitihada zote nayo ikipatikana iwe sababu ya furaha kubwa. Kwa kuwa sisi ni wadhambi pia habari hii ni njema kwetu kwamba Mungu amemruhusu mwanawe atutafute kwa bidii yote katika mradi wake wa ukombozi. Kumbe, tulipotea, Mungu anaingia gharama kututafuta. Basi, tutafutike na tuonekane.
Somo la kwanza linaonyesha hasira ya Bwana dhidi ya Waisraeli waliojiharibu nafsi zao, wakapotoka na kuiacha njia aliyowaamuru, wakajifanyizia ndama ya kuyeyusha, wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakisema ni miungu yao. Mungu akataka kuwaangamiza. Musa alimsihi Bwana asiwawakie hasira bali awakumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wake, ambao aliwaapia kwa nafsi yake kuzidisha kizazi chao mfano wa nyota za mbinguni na kuwaahidia kuwapa nchi hii yote niliyoinena atakipa kizazi chao wairithi. Mungu alisikiliza sala ya Musa akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda Waisraeli.
Somo la pili linaunga mkono kwa uzuri kabisa wazo letu la kwamba tulipotea lakini Mungu anaingia gharama kututafuta. Mtume Paulo anapojitolea mfano mwenyewe kwamba alikuwa kati ya watu wabaya lakini Bwana akamsamehe na kumchagua aingie shambani mwa Bwana. Kwa hiyo, Mtume Paulo anamshukuru Kristo Yesu aliyemtia nguvu kwa sababu alimwona kuwa mwaminifu.
Paulo anasema Yesu alimpatia neema hiyo kwa sababu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi. Kwa maelezo haya, ingekuwa heri na sisi tungetambua tulivyopata rehema kutoka kwa Mungu tukatafutwa na kupatikana. Basi, tuache dhambi na tumtumike Mungu.

SALA: Ee Bwana Yesu Kristo, tunatambua jinsi unavyotushughulikia na jinsi unavyotutafuta kwa bidii ili tusipotee milele. Tutunze tusipotee tena. Amina.