Septemba 10, 2022; Jumamosi: Juma La 23 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: 1 Kor. 10: 14-22

Wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu. Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo. Kikombe kile cha Baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja. Waangalieni hao Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je! Hawana shirika na madhabahu? Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu? Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani. Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani. Au twamtia Bwana wivu? Je! Tuna nguvu zaidi ya yeye?

Wimbo Wa Katikati: Zab. 116: 12-13, 17-18

 1. Nimrudishie Bwana nini
  Kwa ukarimu wake wote alionitendea?
  Nitakipokea kikombe cha wokovu;
  Na kulitangaza jina la Bwana.

K: Nitakutolea dhabihu ya kushukuru, Ee Bwana.

 1. Nitalitakaza jina la Bwana;
  Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
  Naam, mbele ya watu wake wote.
  Katika nyua za nyumba ya Bwana,
  Ndani yako, Ee Yerusalemu. (K)

INJILI: Lk. 6: 43-49

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “ Hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu. Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake. Na kwa nini mnaniita, ‘Bwana, Bwana’ walakini hamyatendi nisemayo? Kila mtu ajaye kwangu, na kuyasikia maneno yangu na kuyatenda, nitawaonyesha mfano wake. Mfano wake ni mtu ajengaye nyumba, na kuchimba chini sana, na kuweka msingi juu ya mwamba; na kulipokuja gharika, mto uliishukia nyumba ile kwa nguvu, usiweze kuitikisa; kwa kuwa imejengwa vizuri. Lakini yule aliyesikia ila hakutenda, mfano wake ni mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi pasipokuwa na msingi, mto ukaishukia kwa nguvu, ikaanguka mara; na maangamizi yake nyumba ile yakawa makubwa.”’

TAFAKARI
TUNDA SAWA NA MTI: Katika Injili ya leo tunajifunza ukweli kuhusu maisha yetu ya kila siku. Maisha ni kama mwangwi. Tukitenda mambo mema yanayotuelezea jinsi tulivyo na tukitenda maovu yanatuelezea jinsi tulivyo pia. Msemo kuwa utavuna ulichopanda unadhihirika katika Injili ya leo. Tujitahidi katika maisha kupanda matendo mema ili tuweze kuvuna yaliyo mema. Yesu anatufundisha kuwa Imani yetu kwa Bwana iendane na matendo yetu. Haitoshi kuungama imani yetu kwa maneno bila matendo, kwani imani bila matendo imekufa (Yak. 2:17). Haitoshi tu kusema mambo mazuri kuhusu Mungu au kumwimbia nyimbo nzuri bali kutekeleza matakwa ya Baba na hivyo kuwa ufunuo wa uwepo wake duniani. Tupo katika ulimwengu uliojaa kila aina ya upepo mbaya na kimbunga kibaya hasa katika mambo yanayohusu imani. Tujenge imani yetu katika mwamba wa sala, Neno la Mungu, Maisha ya Sakramenti, upendo kwa Mungu na jirani. Tukifanya hivyo upepo wa malimwengu hautaweza kututikisa

SALA: Ee Yesu, naomba unijalie niweze kuzaa matunda mema.