Mt. Petro Klaveri, Padre
Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1 1Kor. 9:16-19, 22-27
Ijapokuwa naihubiri injili, sina la kujisifia, maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri injili! Maana nikiitenda kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu; ila ikiwa si kwa hiari yangu, nimeaminiwa uwakili. Basi thawabu yangu ni nini? Ni hii, ya kuwa nihubiripo, nitaitoa injili bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilionao katika injili. Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nalijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi. Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu. Nami nafanya mambo yote kwa ajili ya injili ili kuishiriki pamoja na wengine. Je! Hamjui ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate. Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika. Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa; bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 84: 2-5, 7, 11
- Nafsi yangu imezionea kiu nyua za Bwana,
Naam, na kuzikondea.
Moyo wangu na mwili wangu
Vinamlilia Mungu aliye hai.
K: Maskani zako zapendeza kama nini,
Ee Bwana wa majeshi.
- Shomoro naye ameona nyumba,
Na mbayuwayu amejipatia kioto,
Alipoweka makinda yake,
Kwenye madhabahu zako, Ee Bwana wa majeshi,
Mfalme wangu na Mungu wangu. (K) - Heri wakaao nyumbani mwako,
Wanakuhimidi daima.
Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako,
Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake.
Huendelea toka nguvu hata nguvu,
Huonekana Sayuni kila mmoja mbele za Mungu. (K) - Kwa kuwa Bwana, Mungu, ni jua na ngao,
Bwana atatoa neema na utukufu.
Hatawanyima kitu chema
Hao waendao kwa ukamilifu. (K)
INJILI: Lk. 6:39-42
Yesu aliwaambia wanafunzi wake mithali, “Je! Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili? Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini kila mtu ambaye amehitimu hulingana na mwalimu wake. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi.’”
TAFAKARI
WOKOVU HUANZA NDANI YA MTU: Neno la Mungu linasema “Pasipo maono, watu huacha kujizuia, bali ana heri mtu Yule aishikaye sheria” (Mith 29:18). Katika Injili ya leo tumemsikia Yesu akitahadharisha kuwa kipofu hawezi kumwongoza kipofu mwenzake. Yaani, tunaweza tu kufundisha kile ambacho tumeshakielewa na kukifanya sehemu ya maisha yetu. Kwa mfano wa banzi na boriti Yesu anatufundisha umuhimu wa kufundisha kwa matendo tukianzia ndani mwetu. Ili kuwa viongozi wazuri na waalimu wazuri, ni lazima kuwa na maono sahihi ya wapi tunaenda na nini tunafanya. Kwa kuwa safari yetu ni ya mbinguni, tufuate njia sahihi ambayo ni msalaba wa Kristo, kwa kuwa njia ya msalaba inatupeleka Mbinguni na njia nyingine inatupeleka kwenye shimo la moto wa milele. Tunafundishwa pia tusiwe wepesi wa kuwahukumu wengine kwani hata sisi tunaweza kuwa na madhaifu makubwa zaidi. Tuwe na utayari wa kusahihisha mapungufu yetu na hivyo kuwa mabalozi wa kurekebisha wengine wanapojikwaa.
SALA: Ee Mungu naomba uniongoze katika njia zako. Amina.