Septemba 8,2022; Alhamisi: Juma La 23 La Mwaka

KUZALIWA BIKIRA MARIA MTAKATIFU
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1 Mik. 5:1-4

Bwana asema hivi: “Sasa utajikusanya vikosi vikosi, Ee binti wa vikosi; yeye ametuhusuru; watampiga mwamuzi wa Israeli shavuni mwake kwa fimbo. Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele. Kwa sababu hiyo atawatoa, hata wakati wa kuzaa kwake aliye na utungu; ndipo hayo mabaki ya nduguze watawarudia wana wa Israeli. Naye atasimama, na kulisha kundi lake kwa nguvu za Bwana, kwa enzi ya jina la Bwana, Mungu wake; nao watakaa; maana sasa atakuwa mkuu hata miisho ya dunia.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 13:5-6

  1. Nami nimezitumainia fadhili zako;
    Moyo wangu na uufurahie wokovu wako.

K: Nitafurahi sana katika Bwana.

  1. Naam, nimwimbie Bwana,
    Kwa kuwa amenitendea kwa ukarimu. (K)

INJILI: Mt. 1:1-16, 18-23

Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu. Ibrahimu alimzaaa Isaka; Isaka akamzaa Yakobo; Yakobo akamzaa Yuda na ndugu zake; Yuda akamzaa Peresi na Zera kwa Tamari; Peresi akamzaa Esromu; Esromu akamzaa Aramu; Aramu akamzaa Aminadabu; Aminadabu akamzaa Nashoni; Nashoni akamzaa Salmoni; Salmoni akamzaa Boazi kwa Rahabu; Boazi akamzaa Obedi kwa Ruthu; Obedi akamzaa Yese; Yese akamzaa mfalme Daudi. Daudi akamzaa Sulemani kwa yule mke wa Uria; Sulemani akamzaa Rehoboamu; Rehoboamu akamzaa Abiya; Abiya akamzaa Asa; Asa akamzaa Yehoshafati; Yehoshafati akamzaa Yoramu; Yoramu akamzaa Uzia; Uzia akamzaa Yothamu; Yothamu akamzaa Ahazi; Ahazi akamzaa Hezekia; Hezekia akamzaa Manase; Manase akamzaa Amoni; Amoni akamzaa Yosia; Yosia akamzaa Yekonia na ndugu zake, wakati wa ule uhamisho wa Babeli. Na baada ya ule uhamisho wa Babeli, Yekonia akamzaa Shealtieli; Shealtieli akamzaa Zerubabeli; Zerubabeli akamzaa Abihudi; Abihudi akamzaa Eliakimu; Eliakimu akamzaa Azori; Azori akamzaa Sadoki; Sadoki akamzaa Akimu; Akimu akamzaa Eliudi; Eliudi akamzaa Eleazari; Eleazari akamzaa Matani; Matani akamzaa Yakobo; Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa Yesu aitwaye Kristo.

Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema, Tazama, Bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi.

TAFAKARI
BIKIRA MARIA KATIKA WOKOVU WETU: Leo tunasherehekea sikukuu ya kuzaliwa Bikira Maria. Upo uhusiano wa karibu sana kati ya Bikira Maria na wokovu wetu, kwani ndiye aliyemzaa Mkombozi wetu. Katika Injili tumesikia habari za ukoo wa Yesu Kristo na kuona mpango wa Mungu tangu mwanzo wa kumkomboa mwanadamu. Kwa kujua mtiririko wa ukoo wa Yesu tunapata nafasi ya kumjua Mwokozi wetu. Kuzaliwa kwa Yesu Kristo ni jibu la Mungu kwa matarajio ya Wayahudi na Wapagani ingawa ni kwa njia ya ajabu kabisa. Kama uzao uliotoka kwa Abrahamu, Yesu ni chanzo cha Baraka zote. Mapokeo yanatuambia Bikira Maria alizaliwa na Watakatifu Joachim na Anna. Kuzaliwa kwake katika hali ya Neema na bila dhambi ni ishara ya kuwa Masiha angezaliwa kutoka katika tumbo lake kuja duniani. Tunaposherehekea kuzaliwa Bikira Maria, tumpe heshima anayostahili huyu mama ambaye ni Tabernakulo ya kwanza iliyombeba Mungu.

SALA: Ee Yesu, naomba unijalie Neema ya kumheshimu Mama Bikira Maria. Amina.