Septemba 5, Jumatatu: Juma La 23 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: 1Kor. 5:1-8
Habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye. Nanyi mwajivuna, wala hamkusikitika, ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo. Kwa maana kweli, nisipokuwapo kwa mwili, lakini nikiwako kwa roho, mimi mwenyewe nimekwisha kumhukumu yeye aliyetenda jambo hilo, kana kwamba nikiwapo. Katika jina la Bwana wetu Yesu, ninyi mkiwa mmekusanyika pamoja na roho yangu, pamoja na uweza wa Bwana wetu Yesu; kumtolea Shetani mtu huyo, ili mwili uadhibiwe, ili na roho iokolewe katika siku ya Bwana Yesu. Kujisifu kwenu si kuzuri. Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima? Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo; basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 5:4-6, 11

 1. Unawachukia wote watendao ubatili.
  Utawaaribu wasema wasemao uongo;
  Bwana humzira mwuaji na mwenye hila.

K: Bwana, uniongoze kwa haki yako.

 1. Maana huwi Mungu apendezwaye na ubaya;
  Mtu mwovu hatakaa kwako;
  Wajivunao hawatasimama mbele za macho yako. (K)
 2. Nao wote wanaokukimbilia watafurahi;
  Watapiga daima kelele za furaha.
  Kwa kuwa Wewe unawahifadhi,
  Walipendao jina lako watakufurahia. (K)

INJILI: Lk. 6:6-11

Ilikuwa siku ya sabato nyingine Yesu aliingia katika sinagogi akafundisha; na mlikuwamo mtu ambaye mkono wake wa kuume umepooza. Na waandishi na Mafarisayo walikuwa wakimvizia, ili waone kwamba ataponya siku ya sabato; kusudi wapate neno la kumshitakia. Lakini yeye akayatambua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Ondoka, simama katikati; akaondoka akasimama.” Ndipo Yesu akawaambia, “Nawauliza ninyi, Je! Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya; kuponya roho au kuangamiza?” Akawakazia macho wote pande zote, akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena. Wakajawa na uchungu, wakashauriana wao kwa wao wamtendeje Yesu.

TAFAKARI
NENO LA MUNGU LINAPONYA: Injili ya leo inamwonyesha Yesu akiponya mgonjwa aliyepooza mkono. Bila shaka huyu mgonjwa alitamani sana kuwa mzima tena. Kuponywa mkono uliopooza ni ishara ya ukombozi wa mwanadamu aliyeanguka dhambini na sasa anaponywa na kurudishwa katika hali yake ya awali iliyo na uzima na uzuri wa Kimungu. Kupitia kwa tendo hili la uponyaji, Yesu ameeleza kuwa sabato ni siku ya furaha kama alivyofurahi yule aliyeponywa, siku ya kurudishiwa kilichopotea. Ni siku ya neema ya utakaso bali si mateso. Mmoja wetu anapokuwa na shida, jumuiya nzima inaathirika. Hivyo, wenzetu wanapofanikiwa, tufurahi pamoja nao badala ya kuumia. Tutegemezane daima badala ya kukwamishana iwe ni katika biashara au shughuli yoyote ya kiroho na maendeleo. Yesu amemponya siyo yule aliyepooza mkono tu, ila na wale waliopooza mioyo ambao walitaka asiponywe, nao mioyo yao na akili zao zimeponywa kwa kufundishwa ukweli. Sheria isaidie kuleta furaha na amani siyo kuongeza mahangaiko.

SALA: Ee Yesu, nisaidie niweze kuguswa na shida za wengine niwasaidie. Amina.