Septemba 4,2022; Jumapili: Jumapili Ya 23 Ya Mwaka

MWAKA C
Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Hek. 9:13-19

Ni mtu yupi awezaye kulijua shauri la Mungu? Au ni nani atakayeelewa na mapenzi yake? Kwa kuwa mawazo ya wanadamu yana woga, na makusudi yetu yanaelekea kushidwa; na mwili wenye uharibifu huigandamiza roho, na kiwiliwili cha kidunia huzilemea akili zilizosongwa na masumbuko. Kwa shida tu twayapambanua yaliyoko duniani, na yaliyo karibu nasi ni kazi kuyaona; lakini yaliyoko mbinguni ni nani aliyeyagundua? Naye ni yupi aliyeyavumbua mashauri yako, isipokuwa ulimpa Hekima na kumpelekea Roho yako takatifu kutoka juu? Ndivyo mienendo yao wakaao duniani ilivyosafishwa, na wanadamu walivyofundishwa yakupendezayo; hata na kwa Hekima wao wenyewe waliponywa.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 90:3-6, 12-14, 17

 1. Wamrudisha mtu mavumbini,
  Usemapo, rudini, enyi wanadamu.
  Maana miaka elfu machoni pako
  Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
  Na kama kesha la usiku.

(K) Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu kizazi baada ya kizazi.

 1. Wawagharikisha, huwa kama usingizi,
  Asubuhi huwa kama majani yameayo.
  Asubuhi yachipuka na kumea,
  Jioni yakatika na kukauka. (K)
 2. Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu,
  Tujipatie moyo wa hekima.
  Ee Bwana, urudi, hata lini?
  Uwahurumie watumishi wako. (K)
 3. Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako,
  Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.
  Na uzuri wa Bwana Mungu wetu, uwe juu yetu.
  Na kazi ya mikono yetu uithibitishe. (K)

SOMO 2: Flm. 9:10, 12-17

Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa; ambaye mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya Injili. Lakini sikutaka kutenda neno lo lote isipokuwa kwa shauri lako, ili kwamba wema wako usiwe kama kwa lazima, bali kwa hiari. Maana, labda ndiyo sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele; tokea sasa, si kama mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana; na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika Bwana. Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe.

SHANGILIO Efe. 1:17,18

Aleluya, aleluya,
Ewe Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo,
Uyatie nuru macho ya mioyo yetu,
Ili tujua tumaini la mwito wake jinsi lilivyo.
Aleluya.

INJILI: Lk. 14:25-33

Makutano mengi walipokuwa wakifuatana na Yesu, aligeuka, akawaambia, “Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume kwa wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Mtu yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, ‘Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza. Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali. Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.”’

TAFAKARI
GHARAMA ZA UFUASI ZITALIPA, TUSIZIOGOPE: Wazo hili ni fundisho analotoa Yesu katika kadamnasi yetu hii. Masomo mawili ya mwanzo yapo katika mstari mmoja na Injili yetu. Yesu aliisoma mioyo ya watu walikuwa wakimjia na kutaka kuwa wafuasi wake. Aliwasoma kwamba hakuwa wanampenda kikamilifu wakati ufuasi kwake ulitaka majitoleo makubwa.
Lugha inayotumika inatisha kidogo inaposema mtu asiyewachukia wazazi wake, wanawe, ndugu zake na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wa Yesu. Ukweli ni kwamba katika Kiebrania na Kiaramayo hakuna neno kwa “kupenda nusu au kiasi”. Kuna “kupenda” na “kuchukia” tu. Yesu hakumaanisha kuchukia isipokuwa “kupenda kiasi.”
Hivi anachosema kama mtu hatampenda, hawezi kuwa mwanafunzi wake. Kama sivyo, ingekuwa Yesu anapinga na kubomoa mafundisho yake mwenyewe. Maana ndiye aliyetuachia sisi wanadamu amri ya mapendo kama amri mpya na kuu. (Mt 22:34-40, Yn 13:34-35). Basi kuchukia kuna maana ya kupenda pungufu ukilinganisha na kupendwa kwa Yesu. Kusudi mtu awe mfuasi timamu wa Yesu inampasa kumpenda yeye zaidi.
Wote tunajua jinsi kuwapenda jamaa kulivyo kama tunu yetu Kiafrika. Ni katika mstari huo tuna methali ya “Damu nzito kuliko maji.” Sasa kama ndivyo, basi kumfuasa Yesu kuna gharama na ndizo gharama ambazo tunatakiwa tusiziogope maana “zitalipa”. Baada ya kuonyesha hitaji la kujua gharama ya kumtanguliza yeye katika upendo, Yesu anatoa mifano miwili ya hitaji la kujua. Mfano wa kwanza ni wa mjenga mnara anayepaswa kujua gharama za ujenzi wake asije akakatikiwa na pesa na kushindwa kumaliza ujenzi wake. Mfano wa pili ni wa mtu anayetaka kwenda vitani dhidi ya mtu mwenye askari wengi zaidi kuliko yeye. Huyo naye anatakiwa kujua ukubwa wa jeshi lake kusudi asiende kufanya vita wakati kila hali inaonyesha kwamba atazidiwa. Ndivyo inavyohitaji kujitathimini kabla ya kujidai kutaka kumfuasa Yesu. Ufuasi kwake una gharama lakini gharama ambazo Yesu anataka tusiziogope kwa vile “zitalipa”.
Somo la kwanza linatuama vizuri kwenye haja ya kujua gharama ya jambo badala ya kuliparamia tu. Linasema ingalikuwa vyema sana wanadamu kuweza kuyajua mashauri ya Mungu kabla. Yaani ilifaa sana wanadamu tungeelewa mapenzi ya Mungu kwa sababu hiyo ingalikuwa dawa dhidi ya mawazo yetu ambayo kwa kawaida yametawaliwa na woga, na makusudi yetu yanaelekea kushindwa. Katika hali hiyo miili yetu yenye uharibifu huzigandamiza roho, na viwiliwili vya kidunia hulemea akili zilizosongwa na masumbuko. Kwa namna hii tunaaswa tuyajue mashauri ya Mungu kabla ili tukubali kuwa wafuasi wa Yesu.
Somo la pili linatuonyesha jinsi Paulo anavyomshauri Filemoni aingie kwa hiyari gharama za kumsamehe Onesimo aliyekuwa mtumwa wake akamtoroka. Kwa kadiri ya taratibu za utumwa, ilikuwa Onesimo aadhibiwe vikali kwa kosa la utoro. Lakini kulitokea jambo lililogeuza mambo. Wakati wa utoro wake Onesimo alikutana na Paulo naye akambatiza na kwa kubatizwa Onesimo alifanyika Mkristo sawa sawa na bwana wake. Ndipo hapo Paulo anapomwomba Filemoni ampokee Onesimo si kama mtumwa bali kama Mkristo mwenzake ambaye pamoja naye wana Yesu Kristo kama Bwana na hakimu wao. Paulo anamwambia kwamba hakutaka kutenda neno lo lote pasipo kushauriana naye, ili kwamba wema wake usiwe kama kwa lazima, bali kwa hiari. Kesi hii inaishia vyema kwa Onesimo kusamehewa. Laiti nasi tungeamua mambo kwa busara na siyo papara. Gharama ya kusamehe tutalipwa na Mungu mwenyewe.

SALA: Ee Yesu Kristo, Bwana wetu, tunakuomba tuhimili gharama uupata uzima wa milele. Amina.