Septemba 2,2022; Ijumaa: Juma La 22 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: 1Kor. 4:1-5

Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu. Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu. Lakini, kwangu mimi, si kitu kabisa nihukumiwe na ninyi, wala kwa hukumu ya kibinadamu, wala sijihukumu hata nafsi yangu. Maana sijui sababu ya kujishitaki nafsi yangu, lakini sihesabiwi haki kwa ajili hiyo; ila anihukumuye mimi ni Bwana. Basi ninyi msihukumu neno kabla ya wakati wake, hata ajapo Bwana; ambaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza, na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo; ndipo kila mtu atakapoipata sifa yake kwa Mungu.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 37:3-6, 27, 28, 39-40

  1. Umkabidhi Bwana njia yako.
    Pia umtumaini, naye atafanya.
    Ataitokeza haki yako kama nuru,
    Na hukumu yako kama adhuhuri.

K: Wokovu wa wenye haki una Bwana.

  1. Umtumaini Bwana ukatende mema,
    Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu.
    Nawe utajifurahisha kwa Bwana,
    Naye atakupa haja za moyo wako. (K)
  2. Jiepue na uovu, utende mema,
    Na kukaa hata milele.
    Kwa kuwa Bwana hupenda haki,
    Wala hawaachi watauwa wake. (K)
  3. Na wokovu wa wenye haki una Bwana;
    Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.
    Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa;
    Huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa;
    Kwa kuwa wamemtumaini Yeye. (K)

INJILI: Lk. 5:33-39

Mafarisayo na waandishi walimwambia Yesu, “Wanafunzi wa Yohane hufunga mara nyingi, na kuomba dua; na kadhalika wanafunzi wa Mafarisayo; lakini wanafunzi wako hula na kunywa!” Lakini Yesu akawaambia, “Je! Mwaweza kuwafanya wafunge walioalikwa arusini, akiwapo bwana arusi pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi, ndipo watakapofunga siku zile.” Akawaambia na mithali, “Hakuna akataye kiraka cha vazi jipya na kukitia katika vazi kuukuu; na kama akitia, amelikata lile jipya, na kile kiraka cha vazi jipya hakilingani na lile vazi kuu kuu.

Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama akitia, ile divai mpya itavipasua vile viriba, divai yenyewe itamwagika, na viriba vitaharibika. Lakini divai mpya sharti kutiwa katika viriba vipya. Wala hakuna anywaye divai ya kale akatamani divai mpya; kwa kuwa asema, Ile ya kale ndiyo iliyo njema.”

TAFAKARI
MAISHA MAPYA KATIKA KRISTO: Neno la Mungu leo linatuelezea mabishano kati ya Yesu na viongozi wa dini juu ya suala la kufunga. Kufunga ni zoezi la kiroho la tangu kale ambalo dini nyingi zimesisitiza. Yesu mwenyewe alifunga siku arobaini (Mt.4:2). Hakulazimisha wafuasi wake kufunga bali aliwaacha huru. Uwepo wa Yesu katika maisha ya watu unafananishwa na harusi ambayo washiriki hawafungi bali wanasherehekea. Atakapoondolewa kwao ndipo wataamua kufunga. Divai mpya kwenye viriba vipya na kiraka kipya katika vazi jipya ni lugha ya picha kuonyesha maisha mapya yaliyoletwa na ujio wa Masiya, yanapaswa kubadili mtazamo wetu wa maisha ya kale na kuvaa maisha mapya ya Ukristo. Dini iliyofundishwa na baadhi ya viongozi kwa kiasi fulani ni kama vazi kuukuu, hivyo dini ya Kristo haipaswi kuchanganywa na tamaduni zetu za kale. Dini ya Kristo inaangamiza yale ya kale mfano matambiko na sadaka kwa mizimu. Tusiwe na imani mkorogo inayomshikilia Kristo na wakati huohuo kukumbatia utamaduni usio mzuri.

SALA: Ee Yesu naomba unijalie udumifu katika neema ya ubatizo. Amina.