Septemba 1, 2022; Alhamisi: Juma La 22 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: 1Kor. 3:18-23

Mtu asijidanganye mwenyewe; kama mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe mpumbavu, ili apate kuwa mwenye hekima. Maana hekima ya dunia hii ni upuzi mbele za Mungu. Kwa maana imeandikwa, yeye ndiye awanasaye wenye hekima katika hila yao. Na tena, Bwana anayafahamu mawazo ya wenye hekima ya kwamba ni ya ubatili. Basi, mtu ye yote na asijisifie wanadamu. Kwa maana vyote ni vyenu; kwamba ni Paulo, au Apolo, au Kefa; au dunia, au uzima, au mauti; au vile vilivyopo sasa, au vile vitakavyokuwapo; vyote ni vyenu; nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu.

Wimbo Wa Katikti: Zab. 24:1-6

  1. Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
    Dunia na wote wakaao ndani yake.
    Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
    Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.

K: Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana.

  1. Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
    Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
    Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
    Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili,
    Wala hakuapa kwa hila. (K)
  2. Atapokea Baraka kwa Bwana,
    Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
    Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
    Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K)

INJILI: Lk. 5:1-11

Makutano walipomsonga Yesu wakilisikiliza neno la Mungu, Yeye alikuwa amesimama kando ya ziwa la Genesareti, akaona vyombo viwili vimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka, wanaosha nyavu zao. Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni. Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, “Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue Samaki”. Simoni akajibu akamwambia, “Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.” Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama. Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, “Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana.” Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata; na kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu.” Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata.

TAFAKARI
KUMFUATA KRISTO KWA IMANI: Katika Injili ya leo tumemsikia Yesu akimwita Petro amfuate, ili aendeleze kazi ya kufundisha watu kama Yesu alivyokuwa akifundisha. Kabla ya mwito huu Yesu alikuwa akifundisha watu akiwa kwenye chombo cha uvuvi. Hii inaonyesha kuwa Neno la Mungu linapaswa kufundishwa mahali popote penye watu, siyo lazima jengo kubwa. Yesu alihitaji watu tu ili awafundishe na aliwafuata kule walikokuwa bila kuwasubiri waje kwake. Hii ni changamoto kwa viongozi wetu wa kiroho wawe na utayari wa kuwafuata watu na kuwafundishia pale walipo. Muujiza anaotenda wa kumsaidia Petro kupata samaki wengi unaongeza imani na siyo umaarufu. Wingi wa samaki unamfanya Petro awe mkarimu kwa wengine kwani asingeweza kubeba mzigo wote mwenyewe. Tujifunze kuwa hakuna anayeweza kujitosheleza mwenyewe bila msaada wa wengine na pia mafanikio yetu wenyewe bila kuwashirikisha wengine hayana faida. Ni lazima kusaidiana na kutegemezana katika maisha. Neno la Mungu linawavuta wengi kwa Mungu na linatufanya tujitambue.

SALA: Ee Yesu ninaomba neema ya kuwa mfuasi wako mwaminifu. Amina.