Agosti 31,2022; Jumatano: Juma La 22 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: 1Kor. 3:1-9

Ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa, sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? Maana hapo mtu mmoja asemapo, mimi ni wa Paulo; na mwengine, mimi ni wa Apollo, je! Ninyi si wanadamu? Basi Apollo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apollo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye. Basi yeye apandaye, na yeye atiaye maji ni wa moja, lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa na taabu yake mwenyewe. Maana sisi tu wafanyakazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 33:12-15, 20-21

 1. Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao,
  Watu aliowachagua kuwa urithi wake.
  Toka mbinguni Bwana huchungulia,
  Huwatazama wanadamu wote pia.

(K) Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao,
watu aliowachagua kuwa urithi wake.

 1. Toka mahali pake aketipo
  Huwaangalia wote wakaao duniani.
  Yeye aiumbaye mioyo yao wote
  Huzifikiri kazi zao zote. (K)
 2. Nafsi zetu zinamngoja Bwana;
  Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
  Maana mioyo yetu itamfurahia,
  Kwa kuwa tumelitumainia jina lake takaifu. (K)

INJILI: Lk. 4:38-44

Yesu alitoka katika sinagogi, akaingia katika nyumba ya Simoni. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa ameshikwa na homa kali, wakamwomba kwa ajili yake. Akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, ikamwacha; mara hiyo akaondoka, akawatumikia. Na jua lilipokuwa likichwa, wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi mbali mbali waliwaleta kwake, akaweka mikono yake juu ya kila mmoja akawaponya. Pepo nao waliwatoka watu wengi, wakipiga kelele na kusema, “Wewe u Mwana wa Mungu.” Akawakemea, asiwaache kunena, kwa sababu walimjua kuwa ndiye Kristo. Hata kulipokucha alitoka akaenda mahali pasipokuwa na watu; makutano wakawa wakimtafuta-tafuta, wakafika kwake, wakataka kumzuia asiondoke kwao. Akawaambia, “Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana kwa sababu hiyo nalitumwa. Basi, alikuwa akihubiri katika masinagogi ya Galilaya.”

TAFAKARI
TUTUMIKIE BILA MIPAKA: Bwana wetu Yesu Kristo katika somo la Injili anatufundisha kutumikia bila mipaka na kwa watu wote. Yesu ni Mtumishi wa Bwana aliyekuja kutangaza Habari Njema kwa kila mji na kijiji kuponya, kufundisha na kufukuza pepo. Kutoka kwa Yesu tujifunze tabia ya unyenyekevu. Hajifungamanishi na sehemu moja, labda yenye ukuu na utukufu. Kama Yesu Kristo tunatakiwa kuwa na roho ya kupenda kwenda kutangaza kwa watu wote ujumbe wa kukomboa na wa upendo wa Mungu. Utume wetu kwa watu uwe ni ule usiochagua mahali wala watu. Hilo tunaweza kulitekeleza kwa kuhubiri Upendo ambao mtu yeyote anauelewa bila kujali dhehebu wala dini. Lengo letu liwe ni kuurithi Uzima wa milele ambalo ni lengo letu sote. Aidha, katika kutimiza wajibu wetu, tuweze kuwaponya wenye shida mbalimbali za kimwili na kiroho na kupunguza makali ya magumu ya watu wanaofungwa na vifungo mbalimbali vya kimwili, kiakili na kiroho.

SALA: Ee Mungu, utujalie moyo wa kutumikia bila mipaka na bila kuchoka. Amina.