Agosti 30, 2022; Jumanne: Juma La 22 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: 1Kor. 2:10-16

Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu. Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni. Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu. Maana, Ni nani aliyeifahamu nia ya Bwana, amwelimishe? Lakini sisi tunayo nia ya Kristo.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 145:8-14

 1. Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
  Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema,
  Bwana ni mwema kwa watu wote
  Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote. K: Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote.
 2. Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
  Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
  Wataunena utukufu wa ufalme wako,
  Na kuuhadithia uweza wako.
  Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu,
  Na utukufu wa fahari ya ufalme wake. (K)
 3. Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
  Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote.
  Bwana huwategemeza wote waangukao,
  Huwainua wote walioinama chini. (K)

INJILI: Lk. 4:31-37

Yesu alishuka mpaka Kapernaumu, mji wa Galilaya, akawa akiwafundisha siku ya sabato; wakashangaa mno kwa mafundisho yake, kwa kuwa neno lake lilikuwa na uwezo. Na ndani ya sinagogi mlikuwa na mtu mwenye roho ya pepo mchafu, akalia kwa sauti kuu, akisema, “Acha! Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Nakujua u nani, Mtakatifu wa Mungu.” Yesu akamkemea, akisema, “Fumba kinywa, mtoke.” Ndipo yule pepo akamwangusha katikati, akamtoka asimdhuru neno. Mshangao ukawashika wote, wakasemezana wakisema, “Ni neno gani hili, maana awaamuru pepo wachafu kwa uwezo na nguvu, nao hutoka.” Habari zake zikaenea kila mahali katika nchi ile.

TAFAKARI
FUMBA KINYWA MTOKE: maneno haya makali na yenye amri yanatamkwa na Bwana wetu Yesu Kristo yakionyesha mamlaka yake kama Mwana wa Mungu. Kwa upande mwingine, pepo mchafu alitambua uwepo wa Yesu Kristo, kwamba yuko aliye mkuu na mwenye nguvu kuliko wao ndani ya Sinagogi. Pepo anakiri kwa sauti kuwa Yesu ni Mungu pale asemapo, “Najua u nani, Mtakatifu wa Mungu.” Yesu kweli ana nguvu juu ya uovu, kifo, nguvu za giza na hata pepo ndio maana kwa kutumia maneno anasema, “Fumba kinywa mtoke”. Tumruhusu Kristo aingie kwenye maisha yetu akemee kila aina ya uovu ndani yetu. Nyakati nyingine tunasumbuliwa hata na mambo madogomadogo na kutufanya tukose amani. Katika nyakati kama hizo tumkaribishe Yesu ili aweze kukemea hali mbaya kama hizo. Kwa jinsi hiyo tutakuwa na amani na utulivu katika miyoyo yetu, katika familia na jumuiya zetu na katika maisha yetu kwa ujumla.

SALA: Ee Mungu, utujalie ushupavu wa kukemea maovu katika jamii zetu. Amina