Kufa kwa shahidi Mt. Yohane Mbatizaji
Kumbukumbu
Nyekundu
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: 1Kor. 2:1-5
Ndugu zangu, mimi nilipokuja kwenu, sikuja niwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha wa maneno, wala kwa hekima. Maana naliazimu nisijue neno lo lote kwenu ila Yesu Kristo, naye amesulibiwa. Nami nalikuwako kwenu katika hali ya udhaifu na hofu na matetemeko mengi. Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 119:97-102
- Sheria yako naipenda mno ajabu,
ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa.
Maaagizo yako hunitia hekima kuliko adui zangu,
Kwa maana ninayo siku zote.
(K) Sheria yako, Ee Bwana, naipenda mno ajabu.
- Ninazo akili kuliko wanafunzi wangu wote
Maana shuhuda zako ndizo nizifikirizo.
Ninao ufahamu kuliko wazee,
Kwa kuwa nimeyashika mausia yako. (K) - Nimeiepusha miguu yang una kila njia mbaya,
Ili nilitii neno lako.
Sikujiepusha na hukumu zako,
Maana Wewe mwenyewe umenifundisaha. (K)
INJILI: Lk. 4:16-30
Yesu alienda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.” Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, “Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu.” Wakamshuhudia wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake. Wakasema, “Huyu siye mwana wa Yusufu?” Akawaambia, “Hapana shaka mtaniambia mithali hii, Tabibu, jiponye nafsi yako; mambo yote tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende na hapa pia katika nchi yako mwenyewe.” Akasema, “Amin, nawaambia ya kuwa, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe.” Lakini, kwa hakika nawaambia, “Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Tena, palikuwa na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila Naamani, mtu wa Shamu.” Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo. Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini; lakini yeye alipita katikati yao, akaenda zake.
TAFAKARI
TUMEBATIZWA NA KUTUMWA KUHUBIRI HABARI NJEMA: Yesu alibatizwa na kutumwa kuitangaza Habari Njema kwa watu wote. Kazi ya kutangaza Habari Njema ni ya Roho Mtakatifu. Injili inaonyesha kuwa Yesu ndiye Masiha aliyeahidiwa, na yeye mwenyewe anasoma sehemu ya Maandiko Matakatifu inayomhusu yeye mwenyewe. Watu wa kwake wanamdharau kwa kuwa wanafahamu hasili yake ya kibinadamu. Yesu anawapa mifano ya mjane nyakati za Nabii Eliya huko Sarepta katika nchi ya Sidoni na mfano wa Naaman mtu wa Shamu ambao Mungu aliwachagua miujiza itendeke kwao. Hapo Yesu anawathibitishia kuwa yeye ni Masiha aliyetabiriwa na amekuja kwao ili kuwaokoa. Nasi sasa baada ya kubatizwa tulitumwa kwenda kuhubiri Habari Njema kila mmoja kadiri ya hali na wito wake. Kimsingi sote tunatumwa kuitangaza Habari Njema katika mazingira tunayoishi kwa maneno yetu mema ya kumpendeza Mungu. Tuombe neema ya ufanisi katika utume wetu.
SALA: Ee Mungu, utujalie neema ya kutekeleza utume wetu wa kutangaza Habari Njema. Amina.