Agosti 28, 2022; Jumapili: Jumapili Ya 22 Ya Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: YbS. 3:17-20, 28-29

Mwanangu, wakati wa kufanikiwa uendelee katika unyenyekevu; hivyo utapendwa kuliko mwenye ukarimu. Kadiri ulivyo mkuu uzidi kujinyenyekesha, nawe utapata kibali machoni pa Bwana; kwa maana rehema zake Bwana zi kuu, na siri yake ni kwa wanyenyekevu. Msiba wa mwenye kiburi hauleti kupona, Mche wa uovu umepandika ndani yake. Moyo wa busara utatambua mithali, Na sikio sikivu ni tamaa ya mtaalamu.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 68:3-6, 9-10

 1. Wenye haki watafurahi,
  Na kushangilia uso wa Mungu;
  Naam, watapiga kelele kwa furaha.
  Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake.
  Furahini katika Bwana, shangilieni mbele zake (K) Ee Mungu, Kwa wema wako uliwahifadhi walioonewa.
 2. Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane,
  Mungu katika kao lake takatifu.
  Mungu huwakalisha wapweke nyumbani,
  Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa. (K)
 3. Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema,
  Urithi wako ulipochoka uliutia nguvu.
  Kabila lako lilifanya kao lake huko,
  Ee Mungu,
  Kwa wema wako uliwahifadhi walioonewa. (K)

SOMO 2: Ebr. 12:18-19, 22-24

Hamkufikilia mlima uwezao kuguswa, uliowaka moto, wala wingu jeusi, na giza, na tufani, na mlio wa baragumu na sauti ya maneno; ambayo wale walioisikia walisihi wasiambiwe neno lo lote lingine. Bali ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi, mkutano mkuu na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika, na Yesu mjumbe wa agano jipya.

SHANGILIO: Mt. 11:25

Aleluya, aleluya,
Ninakushukuru Baba, Bwana wa mbingu na nchi, Kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, Ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya.

INJILI: Lk. 14:1, 7-14

Yesu alipoingia ndani ya nyumba ya mtu mmoja miongoni mwa wakuu wa Mafarisayo siku ya sabato, ale chakula, walikuwa wakimvizia. Akawaambia mfano wale walioalikwa, alipoona jinsi walivyochagua viti vya mbele; akisema, “Ukialikwa na mtu arusini, usiketi katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe, akaja yule aliyewaalika wewe na yeye, na kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza kwa haya kushika mahali pa nyuma. Bali ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie, Rafiki yangu, njoo huku mbele zaidi; ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote walioketi pamoja nawe. Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”

Akamwambia na yule aliyemwalika, “Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo. Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu, nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki.”

TAFAKARI
UNYENYEKEVU HUUSHINDA UKARIMU NA MAJIVUNO: Wazo hili linatokana katika Injili ya leo pamoja na masomo mawili yaliyowekwa na mama Kanisa. Baadhi ya Mafarisayo na waandishi wa sheria, walikuwa wanamchukia Yesu. Ndio hao walikuwa wakimtega Yesu kwa namna mbalimbali mintarafu anachofundisha.
Walimwona Yesu kama mtu aliyejitumbukiza katika taaluma ya ualimu pasipo kupitia hatua halisi. Mafarisayo na waandishi wa sheria walikuwa wanasomea takribani miaka thelathini na minane kuwa Mafarisayo au waandishi wa sheria. Si hivyo tu, kilichowakera zaidi ni kwamba alikuwa anawafundisha watu vizuri na kwa uwezo mkubwa kuliko wao na watu walikuwa wanamwajabia na kumpenda sana. Hayo tisa, alikuwa akithibitisha mafundisho yake mazuri kwa miujiza ya aina tano: kuponya wagonjwa, kufufua wavu, kutoa mapepo, kutawala maumbile na kutabiri mambo yajayo.
Wakati ule wa Yesu, kulikuwa na Mafarisayo na waandishi wengi wa sheria. Basi ikawa wao wanamtafuta wamfanye kitu. Lakini Yesu hakuwaogopa na hakuacha kufundisha. Kama ni maneno ya chuki alijua hayatoboi mwili na wala hayamtii mtu asiyeyajali maradhi. Ndipo kila alipokutana nao alitumia fursa hiyo kuwaonya, kuwakanya na kuwapa darasa la jambo fulani. Katika Injili ya leo, Mafarisayo na Yesu wamekutana nyumbani kwa mmoja wa wakuu wa Mafarisayo. Wamealikwa wote. Mafarisayo wanamtega wamnase katika matendo au maneno. Yesu alijua vyema hila yao. Lakini kwa kuwa yeye alikuja ulimwenguni kuziokoa roho za watu, hakuwaogopa akatumia fursa hiyo kuwapa mafundisho mawili: fundisho la unyenyekevu na fundisho la ukarimu usio na masharti.
Kuhusu unyenyekevu aliwapiga dhidi ya kupenda kwao kujionyesha. Katika karamu meza zilipangwa na ukubwa. Kulikuwa na meza kuu kati ya meza mbili kulia na kushoto. Katikati ya meza kuu ndipo alipokaa mkuu wa sherehe. Kutoka alipokaa yeye viti vilipungua hadhi kulia na kushoto. Ukaaji kwenye viti hivyo kulitegemea mkuu wa sherehe alivyoamua na kuwapanga watu. Kumbe, Mafarisayo na waandishi wa sheria walikuwa watu waliolazimisha kwenda kukaa nafasi za mbele kabisa badala ya kuanza kukaa viti vya mwisho ili wakiitwa waende mbele. Kiroja hiki cha Mafarisayo kupenda viti vya mbele ndicho msingi wa fundisho la Yesu kuhusu unyenyekevu. Yesu aliwasisitizia wahusika bora wawe wanajidhili ili wakwezwe kulikuwa kuwa wanajikweza katika hatari ya kudhiliwa. Baada ya fundisho kuhusu unyenyekevu, Yesu anageukia ukarimu. Anasema watu wakitaka kuwa wakarimu, wawe hivyo pasipo kutarajia malipo yoyote.
Somo la kwanza linatuhimiza kila mmoja wetu awe mnyenyekevu hasa anapofanikiwa maana unyenyekevu humfanya mtu aheshimiwe kuliko anavyoheshimiwa mkarimu. Somo linamwomba kila mtu kwa heshima na taadhima, wakati wa kufanikiwa aendelee katika unyenyekevu. Kadiri mtu anavyokuwa mkuu azidi kujinyenyekesha. Kwa maana rehema zake Bwana zi kuu, na siri yake ni kwa wanyenyekevu. Somo halimung’unyi maneno. Linasema wazi kwamba msiba wa mwenye kiburi hauleti kupona.
Somo la pili linaunga mkono haya tunayoambiana kwa kusisitiza kwamba huyo Yesu anayewafundisha dhidi ya kujikweza na dhidi ya ukarimu wenye masharti anastahili kusikilizwa kwa sababu yeye ni mjumbe wa Agano Jipya. Wa kusikilizwa kwa makini ni Yesu Kristo kwa maana ndiye ziliyemfungukia mbingu na watu wote kualikwa kumsikiliza yeye tu (Mk 9:7-8). Tujiepushe na walimu ambao hawafunzi kweli bali wananadi makanisa yao tu. Somo letu sote ni: Unyenyekevu huushida ukarimu wa maonesho. Tusijionyeshe na tuwe wakarimu na tusitegee kulipwa duniani. Malipo yetu halisi yako kwa Mwenyezi Mungu.

SALA: Ee Yesu Kristo, tusaidie tuwe wanyenyekevu na wakarimu kwa wanaohitahji msaada wetu. Amina.