Agosti 25, 2022; Alhamisi: Juma La 21 La Mwaka

Mt. Ludoviko (Lui)/ Mt. Yosefu wa Kalasanzi, Padre
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: 1Kor. 1:1-9

Paulo, aliyeitwa kuwa mtume wa Yesu Kristo kwa mapenzi ya Mungu, na Sosthene ndugu yetu, kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, wale waliotakaswa katika Kristo Yesu, walioitwa wawe watakatifu, pamoja na wote wanaoliitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo kila mahali, Bwana wao na wetu. Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. Namshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu, kwa sababu ya neema ya Mungu mliyopewa katika Kristo Yesu; kwa kuwa katika kila jambo mlitajirika katika yeye, katika maneno yote, na maarifa yote; kama ushuhuda wa Kristo ulivyothibitika kwenu; hata hamkupungukiwa na karama yo yote, mkikutazamia sana kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye atawathibitisha hata mwisho, ili msilaumiwe siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mungu ni mwaminifu ambaye mliitwa na yeye mwingie katika ushirika wa Mwanawe, Yesu Kristo Bwana wetu.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 145:2-7

 1. Kila siku nitakuhimidi,
  Nitalisifu jina lako milele na milele.
  Bwana ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana,
  Wal ukuu wake hautambulikani.

(K) Ee Bwana, nitalihimidi jina lako. Milele na milele.

 1. Kizazi kwa kizazi kitayasifu matendo yako,
  Kitayatangaza matendo yako makuu.
  Nitaifikiri fahari ya utukufu wa adhama yako,
  Na matendo yako yote ya ajabu. (K)
 2. Watu wayataja matendo yako ya kutisha,
  Nami nitausimulia ukuu wako.
  Watalihubiri kumbukumbu la wema wako mkuu.
  Wataiimba haki yako. (K)

INJILI: Mt. 24:42-51

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja. Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo.” Amin, nawaambieni, “Atamweka juu ya vitu vyake vyote. Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, ‘Bwana wangu anakawia; akaanza kuwapiga wajoli wake, na kula na kunywa pamoja na walevi; bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.”’

TAFAKARI
KESHENI! Yesu anatualika tuwe tayari kwa ujio wake, yaani kukesha. Utayari ni muhimu na lazima kwa sababu hatujui siku wala saa atakaporudi. Hivi cha muhimu ni kukesha. Kipindi cha maisha ya mwanadamu kwa kiasi kikubwa ni cha kusubiri. Tunasubiri matukio mazuri na ya kuvutia katika maisha, mfano kumaliza masomo, kufunga, kuweka nadhiri za utawa, kupokea daraja ya Upadre na kupewa cheo katika kazi. Na katika maisha ya kiroho pia tunakumbana na swala la kusubiri ambako kunaendana na uaminifu na matumaini na hivyo tunaalikwa kudumu au kukesha. Yesu anaendelea kuja kwetu katika matukio mbalimbali ya maisha yetu ya kila siku. Anaendelea kuja kwetu kwa njia ya wahitaji. Anaendelea kuja kwetu katika Neno lake na Ekaristi Takatifu. Ni vigumu kutambua ni lini, ni wakati gani na katika mazingira gani. La msingi ni kuwa tayari daima kwa kuishi kadiri ya inavyompendeza Mungu na wanadamu. Tuiishi Amri Kuu ya Mapendo kwa Mungu na Jirani.

SALA: Ee Mungu utujalie moyo wa kujiweka tayari kwa ujio wa mwanao.