Agosti 24,2022; Jumatano: Juma La 21 La Mwaka

MT. BARTOLOMEO, MTUME
Sikukuu
Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: Ufu. 21:9-14

Malaika alinijia akanena nami, akisema, “Njoo huku, nami nitakuonyesha yule Bibi-arusi, mke wa Mwaka-Kondoo.” Akanichukua katika Roho mpaka mlima mkubwa, mrefu, akanionyesha ule mji mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu; mwenye utukufu wa Mungu, na mwangaza wake ulikuwa mfano wa kito chenye thamani nyingi kama kito cha yaspi, safi kama bilauri; ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu, wenye milango kumi na miwili; na katika ile milango malaika kumi na wawili; na majina yameandikwa ambayo ni majina ya kabila kumi na mbili za Waisraeli. Upande wa mashariki milango mitatu; na upande wa kaskazini milango mitatu; na upande wa kusini milango mitatu; na upande wa magharibi milango mitatu. Na ukuta wa mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi majina kumi na mawili ya wale mitume kumi na wawili na Mwana-Kondoo.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 145:10-13, 17-18

 1. Ee Bwana, kazi zote zitakushukuru,
  Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
  Wataunena utukufu wako,
  Na kuuhadithia uweza wako.

(K) Wacha Mungu wataunena utukufu wa ufalme wako, Ee Bwana.

 1. Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu,
  Na ufalme wa fahari ya ufalme wake.
  Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
  Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. (K)
 2. Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
  Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.
  Bwana yu karibu na wote wamwitao,
  Wote wamwitao kwa uaminifu. (K)

INJILI: Yn. 1:45-51

Filipo alimwona Nathanaeli, akamwambia, “:Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti.” Nathanaeli akamwambia, “Laweza neno jema kutoka Nazareti?” Filipo akamwambia, “Njoo uone.” Basi Yesu, akamwona Nathanaeli anakuja kwake, akanena habari zake, “Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake.” Nathanaeli akamwambia, “Umepataje kunitambua?” Yesu akajibu, akamwambia, “Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona.” Nathanaeli akamjibu, “Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli.” Yesu akajibu, akamwambia, “Kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya.” Akawaambia, “Amini, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”

TAFAKARI
NJOO UONE: Binadamu pengine tuna tabia ya kujishirikisha kwa mambo yaliyo mazuri maishani. Filipo baada ya kukutana na Yesu, hakutaka afaidi peke yake furaha na bahati hiyo njema. Anamshirikisha Nathanaeli. Naye anatia shaka kama “Laweza neno jema kutoka Nazareth?” Ndipo Filipo anapomwalika aje amshuhudie kwa macho yake “Njoo uone”. Mapato ya Nathanaeli kukutana na Yesu ni kumkiri kwa kinywa chake kwa maneno mazito kabisa: “Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli.” Nathanaeli anamtambua Yesu kuwa ni Mwalimu (Rabi), Mwana wa Mungu na Mfalme wa Israeli. Kumbe Nathanieli hatua kwa hatua, anamtambua kuwa kutoka Nazareti, Yesu Mwana wa Mungu ameibuka. Ni maneno yaonyeshayo kukua kwa imani yake juu ya Yesu. Nathaneli ni Mtume Bartholomayo ambaye baadaye alikuwa mtu mnyofu sana na alikufa kifo dini akimshuhudia Kristo.

SALA: Ee Mungu, tujalie moyo wa kuwavuta na kuwapeleka watu kwa Yesu ili waweze kumjua Yesu.