Agosti 23,2022; Jumanne: Juma La 21 La Mwaka

Mt. Rosa wa Lima, Bikira
Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: 2Thes. 2:1-3, 14-17

Tunakusihini ndugu kwa habari ya kuja kwake Bwana Wetu Yesu Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake, kwamba msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo. Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu. Bwana aliwaita ninyi kwa injili yetu, ili kuupata utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, ndugu, simameni imara, mkayashike mapokeo mliyofundishwa, ama kwa maneno, ama kwa waraka wetu. Na Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba yetu, aliyetupenda akatupa faraja ya milele na tumaini jema katika neema, awafariji mioyo yenu, na kuwafanya imara katika kila neno na tendo jema.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 96: 10-13

 1. Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki,
  Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike,
  Atawahukumu watu kwa adili.

(K) Bwana anakuja aihukumu nchi.

 1. Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
  Bahari na ivume nav yote viijazavyo.
  Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
  Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha;
  Mbele za Bwana, kwa maana anakuja.
  Kwa maana anakuja aihukumu nchi. (K)
 2. Atahukumu ulimwengu kwa haki,
  Na mataifa kwa uaminifu wake. (K)

INJILI: Mt. 23: 23-26

Yesu alisema, “Ole wenu Waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache. Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia. Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang’anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi.”

TAFKARI
UAMINIFU NA UNYOFU WA NDANI: Uaminifu na unyofu ni ufunguo katika aina yoyote ile ya mahusiano. Makaripio wanayoendelea kuyapokea Waandishi na Mafarisayo yana lengo la kutualika kuwa waaminifu na wanyofu. Maisha yetu ya imani ni aisha halisi na yanapaswa yaonekane hivyo katika uhalisia wake. Maisha yetu ya Kikristo yanatakiwa yasiwe kama mchezo wa kuigiza, yawe halisi na ya kweli. Nyakati fulani iko hatari ya kuishi maisha yetu kwa lengo la kujionyesha kwa watu kwa kutekeleza mambo ambayo si ya lazima, na kuacha yale ya lazima na muhimu katika maisha yetu ya imani. Hali hii huonekana sana katika jamii na taasisi kwa wale watakao kupanda katika madaraka na hadhi. Basi tusiwe wenye kuziba masikio kwenye mafundisho ya Mtume Paulo: “Lakini kama vile tulivyopata kibali kwa Mungu tuwekewe amana Injili, ndivyo tunavyosema: si kama watu wanaompendeza mwanadamu, bali wampendezao Mungu anayetupima mioyo yetu”. (1 Wathesalonike 2:4).

SALA: Ee Mungu, utujalie moyo wa uaminifu na unyofu. Amina.