Agosti 22, 2022; Jumatatu: Juma La 21 La Mwaka

Bikira Maria Malkia
Kumbukumbu
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: 2Thes. 1:1-5, 11-12

Paulo, na Silwano, na Timotheo, kwa kanisa la Wathesalonike, lililo katika Mungu Baba yetu, na Bwana Yesu Kristo. Neema na iwe kwenu, na amani zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana Yesu Kristo. Ndugu, imetupasa kumshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu, kama ilivyo wajibu, kwa kuwa imani yenu inazidi sana, na upendo wa kila mtu kwenu kwa mwenzake umekuwa mwingi. Hata na sisi wenyewe twaona fahari juu yenu katika makanisa ya Mungu kwa ajili ya saburi yenu, na imani mliyo nayo katika adha zenu zote na dhiki mnazostahimili. Ndiyo ishara hasa ya hukumu iliyo haki ya Mungu, ili mhesabiwe kuwa mwastahili kuingia ufalme wa Mungu, ambao kwa ajili yake mnateswa. Kwa hiyo twawaombea ninyi siku zote, ili Mungu wetu awahesabu kuwa mmekustahili kuitwa kwenu, akatimiza kila haja ya wema na kila kazi ya imani kwa nguvu; jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe ndani yenu, nanyi ndani yake, kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 96:1-5

 1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
  Mwimbieni Bwana, nchi yote.
  Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake.

(K) Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
na watu wote habari za maajabu yake.

 1. Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.
  Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
  Na watu wote habari za maajabu yake. (K)
 2. Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kusifiwa sana.
  Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote.
  Maana miungu yote ya watu si kitu,
  Lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu. (K)

INJILI: Mt. 23:13-22

Yesu aliwaambia makutano na wafuasi wake: “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie. Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu; na akiisha kufanyika, mnamfanya kuwa mwana wa jehanum mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe. Ole wenu viongozi vipofu, ninyi msemao, ‘Mtu atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya hekalu, amejifunga.’ Wapumbavu ninyi na vipofu; maana ni ipi iliyo kubwa, ile dhahabu, au ile hekalu liitakasalo dhahabu? Tena, Mtu atakayeapa kwa madhabahu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa sadaka iliyo juu yake, amejifunga. Vipofu ninyi; maana ni ipi iliyo kubwa, ile sadaka, au ile madhabahu iitakasayo sadaka? Basi yeye aapaye kwa madhabahu, huapa kwa hiyo, na kwa vitu vyote vilivyo juu yake. Naye aapaye kwa hekalu, huapa kwa hilo, na kwa yeye akaaye ndani yake. Naye aapaye kwa mbingu, huapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa yeye aketiye juu yake.”’

TAFAKARI
OLE WENU VIONGOZI VIPOFU: Yesu Kristo anakuja kwa makaripio na ukali uliokithiri dhidi ya Waandishi na Mafarisayo ambao walikuwa na tabia mbaya ya unafiki au uzandiki. Kwa kuwa wao katika jamii yao walikuwa ni viongozi, Yesu anawaita, ‘Viongozi vipofu.’ Anawaita wanafiki na wazandiki kwa kuwa walifundisha ukweli lakini hawakutaka kuuishi huo ukweli walioufundisha. Na walilitenda hilo kwa makusudi, yaani bila kufanya jitihada yoyote ya kuishi kile wanachofundisha. Yesu anatumia maneno makali “Ole wenu” akitaka kuonyesha kuchukizwa kwake na tabia ya Waandishi na Mafarisayo, tabia ya unafiki. Pia lilikuwa onyo kwao na kwa jamii nzima kwamba wasiwe na tabia mbaya kama hiyo. Mafundisho haya ya leo ya Yesu yanatupa changamoto na sisi leo yakitutaka ukweli wa imani na kimaadili tunaoufahamu tuishi. Hivi waamini tunatakiwa kuishi na kutangaza Habari Njema katika maisha yetu. Kwa mifano ya maneno na matendo yetu tuwe watangazaji wa Habari Njema kwa wengine.

SALA: Ee Mungu, utujalie viongozi bora na wenye busara, walio tayari kutuongoza kwa upendo na huruma. Amina.