Agosti 21 Jumapili: Jumapili Ya 21 Ya Mwaka C

Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Isa. 66:18-21

Bwana asema hivi, “Nami nayajua matendo yao na mawazo yao; wakati unakuja nitakapokusanya mataifa yote na lugha zote; nao watakuja, nao watauona utukufu wangu. Nami nitaweka ishara kati yao, nami nitawatuma hao waliookoka kwa mataifa, Tarshishi, na Puli, na Ludi, wavutao upinde, kwa Tubali na Yavani, visiwa vilivyo mbali; watu wasioisikia habari yangu, wala kuuona utukufu wangu; nao watahubiri utukufu wangu katika mataifa. Nao watawaleta ndugu zenu wote kutoka mataifa yote, kuwa sadaka kwa Bwana, juu ya farasi, na katika magari, na katika machela, na juu ya nyumbu, na juu ya wanyama wepesi, mpaka mlima wangu mtakatifu Yerusalemu.” asema Bwana. “Kama vile wana wa Israeli waletavyo sadaka yao nyumbani kwa Bwana katika chombo safi. Na baadhi ya hao nitawatwaa kuwa makuhani na Walawi.” asema Bwana.

Wimbo Wa Katikati Zab. 117

  1. Aleluya.
    Enyi mataifa yote, msifuni Bwana,
    Enyi watu wote mhimidini.

(K) Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili.

  1. Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
    Na uaminifu wa Bwana ni wa milele. (K)

SOMO 2: Ebr. 12:5-7, 11-13

Tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi. Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani. Kwa hiyo inyosheni mikono iliyolegea na magoti yaliyopooza, mkaifanyie miguu yenu njia za kunyoka, ili kitu kilicho kiwete kisipotoshwe, bali afadhali kiponywe.

SHANGILIO: Yn. 17:17

Aleluya, aleluya,
Maneno yako ndiyo kweli Ee Bwana,
Ututakase sisi kwa ile kweli.
Aleluya.

INJILI: Lk. 13:22-30

Yesu alikuwa akipita katika miji na vijiji, akifundisha katika safari yake kwenda Yerusalemu. Mtu mmoja akamwuliza, “Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache?” Akawaambia, “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze. Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, ‘Ee Bwana tufungulie,’ yeye atajibu na kuwaambia, ‘Siwajui mtokako,’ ndipo mtakapoanza kusema, ‘Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu. ‘ Naye atasema, ‘Nawaambia, siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu.’ Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje. Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu. Na tazama, wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.”’

TAFAKARI
TUKIZUBAA TUTAKULA KWA MACHO: Hilo ndilo wazo tunaloweza kusema analotutahadharisha Yesu kwalo. Yesu anataka tuamue sasa kubadilika, vinginevyo watupita tuliodhani wanapotea. Watu wa dini mbalimbali wakizisikiliza dhamiri zao wanaweza kutupita kama tumekaa vile. Yesu alitoa mafundisho ya mwelekeo huu alipokuwa anajibu swali la mtu aliyemdodosa kuhusiana na idadi ya watu wanaookolewa. Ilikuwa ni ruksa na kawaida mwalimu au rabi kuulizwa swali au maswali na mtu yeyote na yeye alitakiwa kujibu kwa weledi wake wote.
Yesu alikuwa anaulizwa maswali mengi manyofu sawia na ya kumtega. Kitu cha pekee kwa Yesu, tofauti kabisa na walimu wengineo ilikuwa kwamba yeye alikuwa bingwa wa ajabu wa kusoma mioyo ya watu. Hasa wale waliokuwa wanamuuliza maswali au kujadiliana naye. Swali la idadi ya wanaokoka halikuwa gumu kulijibu maana ilitakiwa kusema tu ama wanaokolewa ni wengi au ni wachache. Yesu alilijua jibu fika kutokana na umungu wake. Hata hivyo, Yesu alijua akijibu kwa namna hiyo, kinaweza kutokea kituko kikubwa kati ya vituko viwili vifuatavyo. Kwa kujibu ni wengi, muulizaji pamoja na wasikilizaji wanaweza kufurahi na kujiambia kwamba wokovu ni kazi rahisi kwa vile wengi “wanavyopasi” maana kitu kigumu hawawezi kufaulu watu wengi. Kwa kujibu ni wachache, muulizaji pamoja na wasikilizaji wanaweza kuvunjika mioyo lakini wakati huo huo wakijisemea kama wanaookoka ni wachache itamaanisha wanaopotea ni wengi na ikiwa ni wengi basi msiba wa wengi si kitu.
Yesu aliyakwepa matokeo ya vizio hivi viwili. Alimtaka muuliza swali pamoja na wasikilizaji wote kuachana na udadisi usio na tija, badala yake wafanye haraka kupigania kupitia mlango mwembamba mioyo yao itaungua kwa huzuni. Watashangaa kumwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nao wenyewe wakiwa wametupwa nje. Zaidi ya hao watashangaa kuwaona watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu. Lakini mshangao wao mkubwa utakuwa kuwaona waliokuwa wakidhaniwa kuwa wa mwisho wakiwa wa kwanza, na wa kwanza wakiwa wa mwisho.
Somo la kwanza linaripoti kwetu jinsi Bwana anavyotaka kufanya. Hana mpango wa kuwabania wengine nafsi mbinguni kana kwamba sisi tuna hati-miliki ya mbingu. Kinyume chake yeye amejipanga kuwaribisha watu wote mbinguni. Somo la pili linasema ili kumpatia nafasi kila mmoja ya kuingia katika uzima wa milele, wakati mwingine Mungu anaruhusu maumivu au adhabu kwa wasio na mwelekeo mnyofu. Anasema nia ya kuruhusu maumivu au adhabu si kuwafuta katika orodha ila ni namna ya kuwaweka sawa wasipotee na hivyo ndivyo baba yeyote anayewapenda watoto wake anavyofanya. Mungu hututendea kama wana; maana kila mwana hurudiwa na baba yake.
Somo linazidi kutubainishia kwamba kila adhabu wakati wake huonekana kuwa kitu cha karaha na cha kusikitisha; lakini baadaye huwaletea waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani. Somo linamalizia kwa kutuasa tusinyong’onyee kwa sababu ya maumivu au adhabu mbalimbali zinazoruhusiwa na Mungu zitupate.

SALA: Ee Mungu tumeelewa jinsi unavyotupenda na kututakia heri ya kutukusanya makaoni mwako. Usituache tukate tamaa katiuka hali yetu ngumu ya maisha.