Agosti 20, 2022; Jumamosi: Juma La 20 La Mwaka

Mt. Bernardo Abati na Mwalimu wa Kanisa
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Eze. 43:1-7

Bwana alinileta mpaka langoni, yaani, lango lile lielekealo upande wa mashariki; na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea kwa njia ya mashariki; na sauti yake ilikuwa kama mshindo wa maji mengi, nayo nchi iling’aa kwa utukufu wake. Na maono niliyoyaona yalikuwa kama maono niliyoyaona nilipokuja kuharibu mji; nayo maono niliyoyaona yalikuwa kama maono niliyoyaona karibu na mto wa Kebari; nikaanguka kifudifudi. Na huo utukufu wa Bwana ukaingia ndani ya nyumba, kwa njia ya lango lile lielekealo upande wa mashariki. Kisha roho ikaniinua, ikanichukua mpaka ua wa ndani; na tazama, utukufu wa Bwana uliijaza nyumba. Nikasikia sauti ya mmoja asemaye nami, itokayo katika nyumba hiyo; na mtu akasimama karibu nami. Akaniambia, “Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi, na mahali pa nyayo za miguu yangu, nitakapokaa kati ya wana wa Israeli milele”.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 85:8-13

 1. Na asikie atakavyosema Mungu Bwana,
  Maana atawaanbia watu wake amani,
  Naam, na watauwa wake pia,
  Bali wasiurudie upumbavu wake pia,
  Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
  Utukufu ukae katika inchi yetu.

(K)Utukufu wa Bwana ukae katika nchi yetu.

 1. Fadhili na kweli zimekutana,
  Haki na amani zimebusiana.
  Kweli imechipuka katika nchi,
  Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)
 2. Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
  Na nchi yetu itatoa mazao yake.
  Haki itakwenda mbele zake.
  Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia.(K)

INJILI: Mt. 23:1-12

Yesu aliwaambia makutano na wanafunzi wake, akasema, “Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; basi, yoyote watakayowaambia, myashike, na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi. Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao. Tena matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu; kwa kuwa hupanua hirizi zao, huongeza matamvua yao; hupenda viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi. Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu. Na yeyote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.”

TAFAKARI
IMANI HAI NA IMARA HUONEKANA KATIKA MATENDO: Injili ya leo ina lengo la kushambulia unafiki wa Mafarisayo ambao walifundisha yaliyo kweli lakini walitenda yasiyo sawa. Kwa kukemea unafiki wa Mafrisayo, ambao wanatakiwa kusikilizwa katika wanayoyafundisha, tunaalikwa kuishi imani hai na imara inayoonekana katika matendo yanayoendana na imani hiyo. Tunatakiwa kwa jinsi hii kujichunguza na kuona kama imani yetu inaoana na maisha yetu. Ni mara ngapi tunaungama imani yetu sahihi lakini tunaishi kinyume na imani hiyo tunayoiungama? Tukumbuke pia kuungama imani na kutoiishi ni unafiki. Kuishi imani yetu si kitu rahisi hivi, muda mwingine tunashindwa na kukata tamaa. Yesu tunayemfuata yupo pamoja nasi. Tumkimbilie kwa sala na majitoleo yetu ili azidi kutujalia neema itakayotusaidia. Tuwe na imani hai na imara ambayo itaonekana wazi katika maisha yetu ya kila siku.

SALA: Ee Mungu, utujalie imani iliyo hai na imara ili tuweze kukutumikia wewe daima. Amina.