Agosti 18, 2022; Alhamisi: Juma La 20 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO I: Eze. 36:23-28

Neno la Bwana lilinijia hivi: “Nitalitakasa jina langu kuu, lililotiwa unajisi katika mataifa, mlilolitia unajisi kati yao; nao mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana,” asema Bwana Mungu, “Nitakapotakaswa kati yenu mbele ya macho yao. Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe. Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda. Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 51:10-13, 16-17

 1. Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
  Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
  Usinitenge na uso wako,
  Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.

(K) Nitawanyunyizia maji safi; Nanyi mtakuwa safi, nitawatakaseni na uchafu wenu wote.

 1. Unirudishie furaha ya wokovu wako;
  Unitegemeze kwa roho ya wepesi.
  Nitawafundisha wakosaji njia zako,
  Na wenye dhambi watarejea kwako. (K)
 2. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,
  Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.
  Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika;
  Ee Mungu, hutaudharau. (K)

INJILI: Mt. 22:1-14

Yesu aliwaambia makuhani na makutano kwa mithali, akisema, “Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi.” Akawatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja arusini; nao wakakataa kuja. Akatuma tena watumwa wengine, akisema, “Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng’ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini. Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake; nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua.” Basi yule mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao. Kisha akawaambia watumwa wake, “Arusi i tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili. Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini.” Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni.
Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi. Akamwambia, “Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi?” Naye akatekewa. Mfalme akawaambia watumishi, “Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.”

TAFAKARI
KARAMU NI TAYARI, NJONI HARUSINI: Mwaliko kwa karamu ya harusi uliwaendea watu wote bila ubaguzi lakini ni wachache waliokubali kuupokea. Karamu ya harusi kama ilivyo katika siku zetu ni wasaa wa shamrashamra na furaha. Ni kawaida ndugu, jamaa, marafiki na wajuani kukusanyika ili kushiriki katika furaha hii kubwa. Wale walioalikwa wanatoa udhuru wa kutohudhuria sherehe ya harusi mmoja akidai kwenda shambani na mwingine kwenye biashara yake, wakimaanisha kuwa sherehe ya harusi si kipaumbele chao. Leo Yesu anatuandalia Karamu katika kila Misa Takatifu. Sharti ni kushiriki tukiwa na hali ya kustahili. Mungu naye anatualika katika furaha yake katika Karamu ya mbinguni. Ili tuweze kustahili kushiriki katika karamu hii ya mbinguni lazima tuwe na vazi la harusi ambalo ni matendo yetu mema. Je, tunapokea mwaliko kwa moyo radhi? Je, tunafanya maandalizi ya kiroho kabla ya kushiriki kwenye Karamu ya Bwana? Na tunajiandaaje kwa karamu ya milele mbinguni?

SALA: Ee Mungu, utujalia tujiandae vema kwa karamu ya hapa duniani na mbinguni. Amina.