Agosti 14, 2022; Jumapili: Jumapili Ya 20 Ya Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Yer. 38:4-6, 8-10

Ndipo wakuu walimwambia mfalme, “Twakuomba, mtu huyu auawe, kwa kuwa aidhoofisha mikono ya watu wa vita, waliobaki katika mji huu, na mikono ya watu wote, kwa kuwaambia maneno kama hayo; maana mtu huyu hawatafutii watu hawa heri, bali shari.” Naye mfalme Sedekia akasema, “Tazama, yu mikononi mwenu; maana mfalme siye awezaye kufanya neno lo lote kinyume chenu.” Basi wakamtwaa Yeremia, wakamtupa katika shimo la Malkiya, mwana wa mfalme, lililo katika uwanda wa walinzi; wakamshusha kwa kamba. Na mle shimoni hamkuwa na maji, ila matope tu; naye Yeremia akazama katika matope hayo. Ebedmeleki akatoka nyumbani mwa mfalme, akamwambia mfalme, akisema,
“Ee Bwana wangu, mfalme, watu hawa wametenda mabaya katika mambo yote waliyomtenda Yeremia, nabii, ambaye wamemtupa shimoni; naye hakosi hatakufa pale alipo, kwa sababu ya njaa; kwa kuwa hapana mkate kabisa katika mji.” Ndipo mfalme akamwamuru Ebedmeleki, mkushi, akisema, “Chukua pamoja nawe watu thelethini; toka hapa, ukamtoe Yeremia shimoni, kabla hajafa.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 40:1-3, 17

 1. Nalimngoja Bwana kwa saburi,
  Akaniinamia akakisikia kilio changu.

(K) Ee Bwana unisaidie hima.

 1. Akanipandisha toka shimo la uharibifu,
  Toka udongo wa utelezi;
  Akaisimamisha miguu yangu mwambani,
  Akaziimarisha hatua zangu. (K)
 2. Akatia wimbo mpya kinywani mwangu,
  Ndio sifa zake Mungu wetu.
  Wengi wataona na kuogopa,
  Nao watamtumaini Bwana. (K)
 3. Nami ni maskini na mhitaji,
  Bwana atanitunza.
  Ndiwe msaada wangu na wokovu wangu,
  Ee Mungu wangu, usikawie. (K)

SOMO 2: Ebr. 12:1-4

Wapenzi, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu, tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu. Hamjafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi.

SHANGILIO: Lk. 19:38

Aleluya, aleluya,
Ndiye Mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana;
Amani mbinguni, na utukufu huko juu.
Aleluya.

INJILI: Lk.12:49-53

Siku ile Yesu aliwaambia makutano: “Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi? Lakini nina ubatizo unipasao kubatizwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe? Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani?” Nawaambia, “La, sivyo, bali mafarakano. Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu. Watafarakana, baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu na mkwewe; mkwe na mkwe mtu.”

TAFAKARI
HATA TUKIWATESA WAJUMBE WA MUNGU, NI LAZIMA TOBA: Wazo hili linatokea kwenye Injili tuliyosomewa hivi punde nalo linaungwa mkono na masomo yanayoisindikiza. Jambo lile tulilolisikia katika Injili ya siku ya kutolewa Bwana hekaluni likisemwa na mzee Simeoni (Lk 2:34-35).
Katika hadhara ya leo, Yesu anawatahadharisha wanadamu akisema neno alilolileta litagonganisha watu. Watu watagawanyika pande mbili, yaani upande wa wanaomkubali na upande wa wasiomkubali na mwishoni mpasuko huo utamwingiza katika mateso na kifo. Mateso na kifo chake ndiyo anayoita “ubatizo” wake au mahali pengine “kikombe cha kunywa”. “Ubatizo” na “kikombe cha kunywa” ni misamiati inayomaanisha mateso katika Biblia.
Katika somo la kwanza wajumbe wa Mungu wanapitia mateso. Ijapokuwa Mungu haghairi mwaliko wake wa watu kutubu. Tunamwona Yeremia akiteswa chini ya Mfalme Sedekia kwa madai ya kudhoofisha mikono ya watu wa vita waliobaki. Lakini Ebedmeleki anamwambia Mfalme Sedekia ukweli wote.
Somo la pili linatuhimiza kumtazama Yesu na kumwiga kwani kukaza kwake nia na kuhimili kwake viunzi vilivyokuwa njiani mwake alishinda kikamilifu. Mwandishi anachora picha tujisikie kuwa watu tunaoshindania medali kwenye uwanja uliofurika watazamaji. Katika mazingira ya enzi za Wagiriki na Warumi, wanariadha walikimbia uchi wa mnyama yaani pasipo nguo yoyote ya kuwaghasi. Hawakuona haya yoyote kwa sababu ya kuitafuta mede.
Mwandishi anatutaka tusiwe na haya, tuvue dhambi tukimbie mashindano ya kiroho pasipo kitu cha kutughasi maungoni. Ndivyo anavyotuambia tukiwa tumezungukwa na wingu kubwa la mashahidi, tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi zituzingazo, tupige mbio kwa saburi katika mashindano ya kiroho yaliyowekwa mbele yetu huku tukimtazama Yesu.
Mwishoni kabisa, tunaombwa tumtafakari sana Yesu aliyeyastahimili mapingamizi makuu ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, tusije tukachoka. Anasema, kwa vyovyote, hatujapambana sana kwani bado hatujafanya vita hata kumwagika damu katika kushindana kwetu na dhambi.
Tukijumlisha kusema ni kwamba hata tukiwatesa wajumbe wa Mungu na viongozi wa kanisa, mwaliko wa toba unabaki pale pale. Kwa ukatili wetu mwito wa toba unahitajika zaidi. Basi, tuacheni tabia ya kupambana na wajumbe wa Mungu na badala yake tutubu dhambi zetu.

SALA: Ee Mungu wetu mwema, tusaidie tuache kuwatesa wajumbe wako bali tupokee hima mwito wa kutubu. Amina.