Agosti 13,2022; Jumamosi: Juma La 19 La Mwaka

Wat. Ponsiani, Baba Mt. na Hipoliti, Padre, Mashahidi
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Eze. 18:1-10, 13, 30-32

Neno la Bwana likanijia tena kusema, “Je! Maana yake ni nini hata mkatumia mithali hii katika Israeli, mkisema, ‘Baba wamekula zabibu mbichi, nao watoto wakatiwa ganzi la meno?’” “Kama mimi niishivyo,” asema Bwana Mungu, “hamtakuwa na sababu ya kuitumia tena mithali hii katika Israeli. Tazama, roho zote ni mali yangu; kama vile roho ya baba ni mali yangu, ndivyo ilivyo roho ya mwana mali yangu, roho ile itendayo dhambi itakufa. Bali kama mtu ni mwenye haki, na kuyatenda yaliyo halali na haki; hakula juu ya milima, wala hakuviinulia macho vinyago vya nyumba ya Israeli, wala hakumtia unajisi mke wa jirani yake, wala hakumkaribia mwanamke wakati wa kutengwa kwake; wala hakumdhulumu mtu, bali amemrudishia mdeni wake rehani yake, wala hakumnyang’anya mtu mali yake kwa nguvu, naye amewapa wenye njaa chakula chake, na kuwavika nguo walio uchi; ambaye hakumkopesha mtu ili apate faida, wala hakupokea ziada ya namna yo yote; naye ameuepusha mkono wake na uovu, na kufanya hukumu ya haki kati ya mtu na mwenzake; tena ikiwa amezifuata sheria zangu, na kuzishika hukumu zangu; mtu huyu ni mwenye haki; hakika ataishi.” asema Bwana Mungu. “Walakini akizaa mwana aliye mnyang’anyi, mmwaga damu, atendaye mambo hayo mojawapo, naye amekopesha watu ili apate faida, na kupokea ziada; je! Ataishi baada ya hayo? La, hataishi; amefanya machukizo hayo yote; hakika atakufa; damu yake itakuwa juu yake. Basi, nitawahukumu ninyi, nyumba ya Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya njia zake.” asema Bwana Mungu. “Rudini, mkaghairi, na kuyaacha makosa yenu yote; basi hivyo uovu wenu hautakuwa uharibifu wenu. Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa; jifanyieni moyo mpya na roho mpya; mbona mnataka kufa, enyi nyumba ya Israeli? Maana mimi sikufurahii kufa kwake afaye.” asema Bwana Mungu; “basi ghairini, mkaishi.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 51:10-13, 16-17

 1. Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
  Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
  Usinitenge na uso wako,
  Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.

(K) Ee Mungu, uniumbie moyo safi.

 1. Unirudishie furaha ya wokovu wako;
  Unitegemeze kwa roho ya wepesi.
  Nitawafundisha wakosaji njia zako,
  Na wenye dhambi watarejea kwako. (K)
 2. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,
  Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.
  Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika;
  Moyo uliovunjika na kupondeka,
  Ee Mungu, hutaudharau. (K)

INJILI: Mt. 19:13-15

Yesu aliletewa watoto wadogo ili aweke mikono yake juu yao na kuwaombea; wanafunzi wake wakawakemea. Lakini Yesu akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao.” Akaweka mikono yake juu yao, akatoka huko.

TAFAKARI
WATOTO NI ZAWADI NA BARAKA KUTOKA KWA MUNGU: Kutoka kipindi cha Agano la Kale hata sasa, familia zisizojaliwa kupata watoto huwa ni changamoto kwa familia yenyewe na jamii kwa ujumla. Ilikuwa desturi ya tangu kale watoto kuwapeleka kwa Marabi wapate kuwabariki. Ndio maana Yesu aliletewa watoto ili aweke mikono yake juu yao na kuwaombea. Katika kipindi cha Yesu, watoto walikuwa wakidharauliwa na kuwekwa kando ya jamii, kitendo tuonacho wakikitenda wanafunzi wake Yesu. Yesu anawakemea. Injili ya leo inaonyesha Yesu akibadili mtazamo huu finyu na potofu pale anapowaalika watoto waende kwake. Anawabariki na kuwaweka kwenye mstari wa mbele katika Ufalme wa Mbinguni. Yesu Kristo ni Mkombozi wa watu wote, wadogo kwa wakubwa, waume kwa wake, wenye taaluma ya juu na wasio na taaluma. Aidha, tabia ya watoto kuwaamini na kuwategemea wazazi wao ni mfano wa waamini wanaomtegemea Mungu aliye Baba mwenye mapendo makubwa kwa sisi watoto wake.

SALA: Ee Mungu, uzijalie familia zetu ustawi kwa kuwalea watoto katika imani na maadili bora. Amina.