Agosti 12,2022;Ijumaa: Juma La 19 La Mwaka

Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Eze. 16:1-15, 60, 63

Bwana Mungu asema hivi; “Nitakutenda vile vile kama ulivyotenda, uliyekidharau kiapo kwa kulivunja agano. Walakini nitalikumbuka agano langu nililolifanya pamoja nawe, katika siku za ujana wako, nami nitaweka imara agano la milele pamoja nawe. Hapo ndipo utakapozikumbuka njia zako, na kutahayarika, hapo utakapowakaribisha maumbu yako, walio wakubwa wako na wadogo wako; nami nitakupa hao wawe binti zako, lakini si kwa agano lako. Nami nitaweka imara agano langu nawe; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi Bwana; upate kukumbuka, na kufadhaika, usifumbue kinywa chako tena, kwa sababu ya aiba yako; hapo nitakapokusamehe yote uliyoyatenda,” asema Bwana Mungu.

Wimbo Wa Katikati: Isa. 12:2-6

 1. Tazama , Mungu ndiye wokovu wangu;
  Nitatumaini wala sitaogopa;
  Maana Bwana Yehova ni nguvu zangu
  na wimbo wngu;
  naye amekuwa wokovu wangu.

(K) Hasira yako imegeukia mbali, nawe unanifariji moyo.

 1. Basi, kwa furaha mtateka maji
  Katika visima vya wokovu.
  Na katika siku hiyo mtasema,
  “Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
  Litajeni jina lake kuwa limetukuka.” (K)
 2. “Mwimbieni Bwana; kwa kuwa ametenda makuu;
  Na yajulikane haya katika dunia yote.
  Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni;
  Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.” (K)

INJILI: Mt. 19:3-12

Mafarisayo walimwendea Yesu wakamjaribu, wakimwambia, “Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu?” Akajibu, akawaambia, “Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, ‘Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja.”’ Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe. Wakamwambia, “Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha?” Akawaambia, Musa, “Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi.” Nami nawaambia ninyi, “Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini.” Wanafunzi wake wakamwambia, “Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa.” Lakini yeye akawaambia, “Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa. Maana wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee.”

TAFAKARI
BASI ALIOWAUNGANISHA MUNGU, MWANADAMU ASIWATENGANISHE: Mahusiano kati ya mume na mke yanaaza tangu kuumbwa kwao kama tusomavyo katika Kitabu cha Mwanzo. Maneno haya ya Bwana wetu Yesu Kristo yanatupatia muhtasari wa Mafundisho juu ya Ndoa Takatifu katika Maandiko Matakatifu. Yana lengo la kutupatia ufafanuzi kwamba: Ndoa ni muungano mtakatifu na thabiti kati ya mume na mke; tena ni ushirika mtakatifu kati ya wenzi wawili walio sawa; na isitoshe ni zawadi kutoka kwa Mungu; na zaidi sana, Ndoa iliwekwa na Mungu kuwa agano la milele. Kila mmoja huwajibika, kwa ajili ya mwili huu mmoja. Muungano huu mtakatifu wa ndoa ni wa kudumu. Na huu ni mpango wa Mungu ambao unatakiwa ulindwe na kuheshimiwa daima.

SALA; Ee Mungu, uwajalie wanandoa neema ya kudumu katika Agano la Ndoa takatifu. Amina.