Agosti 11,2022; Alhamisi: Juma La 19 La Mwaka

Mt. Klara, Bikira
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Eze. 12:1-12

Neno la Bwana likanijia tena, kusema, “Mwanadamu, wewe unakaa kati ya nyumba iliyoasi, watu ambao wana macho ya kuona, ila hawaoni, wana masikio ya kusikia, ila hawasikii; kwa maana ni nyumba iliyoasi. Basi, mwanadamu, funga tayari vyombo kwa uhamisho, ukahame wakati wa mchana mbele ya macho yao; nawe utahama toka mahali pako hapa mpaka mahali pengine mbele ya macho yao; labda watafahamu, wajapokuwa ni nyumba iliyoasi. Nawe utatoa vyombo vyako, wakati wa mchana, mbele ya macho yao, kana kwamba ni vyombo vya kuhamishwa; nawe mwenyewe utatoka, wakati wa jioni, mbele ya macho yao, kama watu watakavyo katika kuhamishwa. Toboa mahali ukutani mbele ya macho yao, ukachukue vitu kwa kuvipitisha pale. Mbele ya macho yao utajitwika begani pako, na kuvichukua nje gizani; utafunika uso wako, hata usiione nchi, kwa maana nimekuweka uwe ishara kwa nyumba ya Israeli. Nikafanya vile vile kama nilivyoamriwa; nalitoa vyombo vyangu wakati wa mchana kana kwamba ni vyombo vya kuhamishwa, na wakati wa jioni nikautoboa ukuta kwa mkono wangu; nikavitoa gizani, nikavichukua begani, mbele ya macho yao.” Asubuhi neno la Bwana likanijia kusema, “Mwanadamu, nyumba ya Israeli, je! Nyumba ile iliyoasi, hawakukuambia, unafanya nini wewe? Waambie, ‘Bwana Mungu asema hivi; ufunuo huu wamhusu mkuu wa Yerusalemu, na nyumba yote ya Israeli walio kati yao. Sema, Mimi ni ishara kwenu; kama mimi nilivyotenda, wao nao watatendwa vile vile; watahamishwa, watakwenda kufungwa. Naye mkuu aliye kati yao atachukua begani katika giza; naye atatoka kwenda zake; watatoboa mahali ukutani, wapate kuvichukua vyombo vyao nje; atafunika uso wake, kwa sababu hataiona nchi kwa macho yake.”’

Wimbo Wa Katikati: Zab. 78:56-59, 61-62

 1. Walimjaribu Mungu Aliye juu wakamwasi.
  Wala hawakuzishika shuhuda zake.
  Bali walirudi nyuma, wakahaini kama baba zao;
  Wakaepea kama upinde usiofaa.

(K) Usiyasahau matendo ya Mungu.

 1. Wakamkasirisha kwa mahali pao pa juu,
  Wakamtia wivu kwa sanamu zao,
  Mungu akasikia, akaghadhibika,
  Akamkataa Israeli kabisa. (K)
 2. Akaziacha nguvu zake kutekwa,
  Na fahari yake mkononi mwa mtesi.
  Akawatoa watu wake wapigwe kwa upanga;
  Akaughadhibu urithi wake. (K)

INJILI: Mt. 18:21-19:1

Petro alimwendea Yesu akamwambia, “Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba?” Yesu akamwambia, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake. Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni.” Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, ‘Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia.’ Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni.” Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia; akamkamata, akamshika koo, akisema, “Nilipe uwiwacho.” Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, “Nivumilie, nami nitakulipa yote pia.” Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, “Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe?” Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.” Ikawa Yesu alipomaliza maneno hayo, akatoka Galilaya akafika mipaka ya Uyahudi, ng’ambo ya Yordani.

TAFAKARI
MSAMAHA WA KIKRISTO HAUNA KIKOMO: Katika sala ya Baba Yetu tunasali “Utusamehe Makosa yetu, kama na sisi tunavyowasamehe wale wanaotukosea”. Swali la msingi kwa upande wetu ni hili: ni kweli tunawasamehe wale waliotukosea? Petro anapotaja idadi ya saba anajiona kuwa amepiga hatua kubwa katika kiwango cha kusamehe sababu amepita mara mbili ya kiwango cha kawaida cha kusamehe, yaani mara tatu, jumlisha moja. Namba saba ni alama ya ukamilifu. Kumbe Yesu anataka tusamehe saba mara sabini ambayo ni mara 490. Hapo ndipo tunapoupata ukweli kwamba Msamaha wa Kikristo hauna kikomo. Tukumbuke kwamba Yesu mwenyewe anatufundisha kwamba “Haki yenu isipozidi ile ya Waandishi na Mafarisayo hamtaingia katika ufalme wa mbinguni” (Matayo 5:20). Hivi kwa mfano wa Mtumwa aliyesamehewa deni na yeye kushindwa kumsamehe mjoli wake tunafundishwa kusamehe kutoka moyoni, na tuepuke jela tunamowafunga wale waliotukosea kwa kutowasamehe. Tuombe kujaliwa moyo wa kusamehe bila mipaka.

SALA: Ee Mungu, utujalie moyo wa kusamehe na kuhurumia, Amina.