Agosti 10,2022; Jumatano: Juma La 19 La Mwaka

MT. LAURENTI, SHEMASI NA SHAHIDI
Sikukuu
Nyekndu
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: 2Kor. 9:6-10

Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika tendo jema; kama ilivyoandikwa, ametapanya, amewapa maskini, haki yake yakaa milele. Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 112:1-2, 4, 9

  1. Heri mtu yule amchaye Bwana,
    Apendezwaye sana na maagizo yake.
    Wazao wake watakuwa hodari duniani;
    Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.

(K) Heri atendaye fadhili na kukopesha.

  1. Nuru huwazukia wenye adili gizani;
    Ana fadhili na huruma na haki. (K)
  2. Amekirimu, na kuwapa masikini,
    Haki yake yakaa milele,
    Pembe yake itatukuzwa kwa utukufu.(K)

INJILI: Yn. 12:24-26

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amin, amin, nawaambia, “Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi. Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele. Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia,
Baba atamheshimu.”

TAFAKARI
UKARIMU KATIKA KUTOA NI HAZINA: Mtume Paulo analeta utaalamu katika swala la kilimo akilihusisha na swala la ukarimu katika kutoa. Wale wakulima walio wapumbavu wanaoshindwa kutumia akili katika kupanda watavuna haba, bali wale wapandao kwa kutumia akili, yaani kwa kanuni za kilimo bora, watavuna kutosha. Vivyo hivyo, wale watumiao mali zao walizopewa zawadi na Mungu kwa ubahili na uchoyo hao hawatapata thawabu. Bali wale watoao kwa ukarimu kwa wahitaji hao watapata thawabu. Utoacho ni kama mbegu ambayo utapata mavuno yake kwa kadiri ulivyopanda. Kama wasemavyo Waswahili: “Utavuna ulichopanda”. Vivyo hivyo matendo yetu mema ni kama mbegu tuipandayo na tutavuna tulichopanda. Tukipenda nafsi yetu zaidi (uchoyo na ubinafsi) tutakuwa tunajiangamiza maana hatuweki akiba yoyote kwa maisha yetu ya baadaye, bali yatupasa kuichukia nafsi yetu katika ulimwengu huu ili tuisalimishe hata uzima wa milele kwa kuwa wakarimu ili kujiwekea hazina mbinguni.

SALA: Ee Mungu, nijalie moyo wa ukarimu, nijiwekee hazina mbinguni. Amina.