Agosti 9,2022; Jumanne: Juma La 19 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Eze. 2:8-3:4

Ezekieli aliisikia sauti, ikamwambia: “Mwanadamu, sikia neno hili ninalokuambia; usiwe wewe mwenye kuasi kama nyumba ile yenye kuasi; funua kinywa chako, ule nikupacho.” Nami nilipotazama, mkono ulinyoshwa kunielekea; na tazama, gombo la chuo lilikuwa ndani yake. Akalikunjua mbele yangu; nalo lilikuwa limeandikwa ndani na nje; ndani yake yalikuwa yameandikwa maombolezo, na vilio, na ole! Akaniambia, mwanadamu, “Kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli.” Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo. Akaniambia, “ Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo.” Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali.” Akaniambia, “Mwanadamu, haya! Waendee wana wa Israeli, ukawaambie maneno yangu.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 119:14, 24, 72, 103, 111, 131

 1. Nitalitangaza jina Bwana;
  Mpeni ukuu Mungu wetu.
  Yeye mwamba, kazi yake ni kamilifu;
  Maana, njia zake zote ni haki.
  Mungu wa uaminifu, asiye na uovu,
  Yeye ndiye mwenye haki na adili.

(K) Mausia yako matamu sana kwangu.

 1. Kumbuka siku za kale,
  Tafakari miaka ya vizazi vingi;
  Mwulize baba yako, naye atakuonyesha;
  Wazee wako, nao watakuambia. (K)
 2. Yeye Aliye juu alipowapa mataifa urithi wao,
  Alipowabagua wanadamu,
  Aliweka mipaka ya watu
  Kwa kadiri ya hesabu ya wana wa Israeli.
  Maana, sehemu ya Bwana ni watu wake,
  Yakobo ni kura ya urithi wake. (K)
 3. Bwana peke yake alimwongoza,
  Wala hapakuwa na mungu mgeni pamoja naye. (K)

INJILI: Mt. 18:1-5, 10, 12, 14

Wanafunzi walimwendea Yesu wakisema, “Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao,” akasema, “Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, yeyote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni. Na yeyote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi. Angalieni msidharau mmojawapo wa wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika zao mbinguni sikuzote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni. Mwaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, mmoja akampotea, je! Hawaachi wale tisa na tisini, akaenda milimani, na kumtafuta yule aliyepotea? Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee.”

TAFAKARI
TABIA ZA MTOTO KAMA MSAADA KATIKA KUURITHI UFALME WA MBINGUNI: Hamu na matamanio ya ukubwa na cheo yalikuwako hata miongoni mwa wanafunzi wa Yesu, kama ilivyo miongoni mwetu leo. Hilo linadhihirika wazi kwenye Injili ya Marko (10:37) pale Yakobo na Yohane wanapoonyeshwa kwenda kwa Yesu kuomba waketi upande wa kuume na kushoto katika ufalme wake. Katika Injili ya leo kwa mshangao anamweka mbele ya wanafunzi wake mtoto mdogo kuwa mfano wa ukuu katika ufalme wa mbinguni. Pamoja na mtoto kutohesabika kati ya watu na kuonekana kuwa dhaifu mbele ya watu, Yesu anamuweka katikati ya kusanyiko kuwa mfano wa kuigwa na wote watakao kuingia kwenye ufalme wa mbinguni. Kwa mtoto tunajifunza hali za uaminifu, unyenyekevu, uwazi, kutumaini na kutegemea. Hali hizi zikielekezwa kwa Mungu katika uaminifu wote basi tutastahilishwa kuingia kwenye ufalme wa mbinguni.

SALA: Ee Mungu utujalie moyo wa unyenyekevu na kukutegemea wewe ili tuweze kuurithi ufalme wa mbinguni. Amina.