Agosti 8,2022; Jumatatu: Juma La 19 La Mwaka

Dominiko, Padre
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Eze. 1:2-5, 24-28

Siku ya tano ya mwezi, nao ulikuwa ni mwaka wa tano wa kuhamishwa kwake mfalme Yehoyakini, neno la Bwana lilimjia Ezekieli, kuhani, mwana wa Buzi, kwa dhahiri, katika nchi ya Wakaldayo, karibu na mto Kebari. Na mkono wa Bwana ulikuwa hapo juu yake. Nikaona, na tazama, upepo wa dhoruba ulitoka upande wa kaskazini, wingu kubwa sana, pamoja na moto, ukifanya duara ya nuru, na mwangaza pande zote, na katikati yake kitu kama rangi ya kaharabu, katikati ya moto huo. Kukatokea katikati yake mfano wa viumbe hai vinne. Kuonekana kwao kulikuwa hivi; walikuwa na sura ya mwanadamu. Nao walipokwenda nalisikia mshindo wa mabawa yao, kama mshindo wa maji makuu, kama sauti yake Mwenyezi, mshindo wa mvumo, kama mshindo wa jeshi; hapo waliposimama walishusha mabawa yao. Tena palikuwa na sauti juu ya anga lile, lililokuwa juu ya vichwa vyao; hapo waliposimama walishusha mabawa yao. Na juu ya anga, lililokuwa juu ya vichwa vyao, palikuwa na mfano wa kiti cha enzi, kuonekana kwake kama yakuti samawi; na juu ya mfano huo wa kiti cha enzi, ulikuwako mfano kama kuonekana kwa mfano wa mwanadamu juu yake. Nikaona kana kwamba ni rangi ya kaharabu, kama kuonekana kwa moto ndani yake pande zote, tangu kuonekana kwa viuno vyake na juu; na tangu kuonekana kwa viuno vyake na chini, naliona kana kwamba ni kuonekana kwa moto; tena palikuwa na mwangaza pande zake zote. Kama kuonekana kwa upinde wa mvua, ulio katika mawingu siku ya mvua, ndivyo kulivyokuwa kuonekana kwa mwangaza ule pande zote. Ndivyo kulivyokuwa kuonekana kwake mfano huo wa utukufu wa Bwana. Nami nilipoona nalianguka kifudifudi.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 148:1-2, 11-14

 1. Aleluya.
  Msifuni Bwana kutoka mbinguni,
  Msifuni katika palipo juu.
  Msifuni, enyi malaika zake wote;
  Msifuni, majeshi yake yote.

(K) Utukufu wako unajaza mbingu na ulimwengu.

 1. Wafalme wa dunia, na watu wote,
  Wakuu, na makadhi wote wa dunia.
  Vijana waume, na wanawali.
  Wazee, na watoto. (K)
 2. Na walisifu jina la Bwana,
  Maana jina lake peke yake limetukuka;
  Adhama yake I juu ua nchi na mbingu. (K)
 3. Naye amewainulia watu wake pembe,
  Sifa za watauwa wake wote;
  Wana wa Israeli, watu walio karibu naye.
  Aleluya. (K)

INJILI: Mt. 17:22-27

Mitume walipokuwa wakikaa Galilaya, Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua, na siku ya tatu atafufuka.” Wakasikitika sana. Hata walipofika Kapernaumu, wale watozao nusu-shekeli walimwendea Petro, wakasema, “Je! Mwalimu wenu hatoi nusu-shekeli?” Akasema, “Hutoa.” Naye alipoingia nyumbani, Yesu alitangulia kumwuliza, akisema, “Waonaje, Simoni? Wafalme wa dunia hutwaa kodi ama ushuru kwa watu gani? Kwa wana wao au kwa wageni?” Naye aliposema, “Kwa wageni.” Yesu alimwambia, “Basi, kama ni hivyo, wana ni mahuru. Lakini tusije tukawakwaza, enenda baharini ukatupe ndoana, ukatwae samaki yule azukaye kwanza; na ukifumbua mdomo wake utaona shekeli; ichukue hiyo ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako.”

TAFAKARI
WAJIBU WETU KWA SERIKALI: Kila muumini aliye katika ufalme wa Mungu, pia ni raia katika nchi yake. Moja kati ya wajibu wa raia katika nchi ni kushiriki katika mambo yanayohusu kustawisha na kujenga taifa lake mintarafu swala zima la uchumi. Wayahudi wote wanaume wenye umri wa kuanzia miaka 20 na kuendelea waliwajibika kulipa nusu-shekeli kila mwaka (Kutoka 30:11-16). Kiasi hiki kilikuwa sawa na ujira wa siku mbili kwa mfanyakazi wa kawaida. Japokuwa Yesu hakuwajibika kulipa (mahuru) kwa hoja ya kuepuka makwazo anaamuru ilipwe kwa ajili yake na Petro. Fedha hii ilitumika kwa ajili ya huduma kwa jamii na utunzaji wa hekalu. Hapo Yesu anatoa fundisho la wazi juu ya wajibu wetu wa kutegemeza serikali na umuhimu wa ushiriki wetu katika mambo yanayohusu maendeleo ya jamii. Wajibu huu unagusa makundi ya Makleri, Watawa na Walei. Tusikwepe wajibu huu kwa hoja au ujanja wowote.

SALA: Ee Mungu, wewe ndiye unayeweka mamlaka za dunia, upende kuzibariki serikali zetu, na uwape viongozi wetu hekima na busara ya kuongoza nchi zetu kwa haki na amani. Amina.