Agosti 6, 2022; Jumamosi: Juma La 18 La Mwaka

KUNG’ARA B. W. YESU KRISTU
Sikukuu
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: Dan. 7:9-10, 13-14

Mimi nilitazama hata viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao. Mto kama wa moto ukapita mbele zake; maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa. Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo haitapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 97:1-2, 5-6, 9

 1. Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie,
  Visiwa vingi na vifurahi.
  Mawingu na giza vyamzunguka,
  Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake.

(K) Bwana ametamalaki, juu sana kuliko nchi yote.

 1. Milima iliyeyuka kama nta mbele za Bwana
  Mbele za Bwana wa dunia yote.
  Mbingu zimetangaza haki yake,
  Na watu wote wameuona utukufu wake. (K)
 2. Maana wewe, Bwana, ndiwe uliye juu,
  Juu sana kuliko nchi yote;
  Umetukuka sana juu ya miungu yote. (K)

SOMO 2: 2 Pet. 1:16-19

Hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake. Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, huyo ni mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu. Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing’aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu.

INJILI: Lk. 9:28-36

Yesu aliwatwaa Petro na Yohane na Yakobo, akapanda mlimani ili kuomba. Ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta. Na tazama, watu wawili walikuwa wakizungumza naye, nao ni Musa na Eliya; walioonekana katika utukufu, wakanena habari za kufariki kwake atakakotimiza Yerusalemu.

Petro na wale waliokuwa pamoja naye walikuwa wamelemewa na usingizi; lakini walipokwisha amka waliuona utukufu wake, na wale wawili waliosimama pamoja naye. Ikawa hao walipokuwa wakijitenga naye, Petro akimwambia Yesu, “Bwana mkubwa ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu; kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya; hali hajui asemalo.”

Alipokuwa akisema hayo, lilitokea wingu likawatia uvuli, wakaogopa walipoingia katika wingu hilo. Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, “Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye.” Na sauti hiyo ilipokwisha, Yesu alionekana yu peke yake. Nao wakanyamaza wasitangaze kwa mtu siku zile lo lote katika hayo waliyoyaona.

TAFAKARI
TUMSIKILIZE YESU: Sauti ya Baba katika tukio la Yesu kung’ara sura mbele ya Petro, Yakobo na Yohane kulikuwa na lengo la Yesu kuwadhihirishia Mitume hawa utukufu wake. Pia kuwatia moyo na kuwaandaa ili wasije wakakwazwa pale watakapomuona Bwana wao akifa Msalabani, watambue kuwa baada ya mateso kuna utukufu. Ni kama wasemavyo Waswahili, “Baada ya dhiki faraja.” Mitume kwa upande wao wanavutiwa na kunogewa na hali ile ya utukufu, hata wanapendekeza wajenge vibanda vitatu cha Yesu, Eliya na Musa. Sauti ya Baba inaleta mwongozo wa Mitume “kumsikiliza Yesu”. Badala ya kujiamulia na kujipangia wafanye nini, wanatakiwa wamsikilize Yesu anavyosema. Nasi leo, Yesu anaendelea kuongea nasi kwa njia mbalimbali. Inatupasa kumsikiliza. Sauti ya Baba inaendelea kusikika mioyoni mwa kila mmoja wetu ambaye kwa ubatizo amekuwa mwana Mpendwa na Mteule wa Mungu ikisema “Msikieni yeye”. Tumsikilize Yesu kwa yote anayotuambia.

SALA: Ee Yesu, utujalie moyo wa kuisikia sauti yako na kuishi kulingana na mafundisho yako. Amina.