Agosti 5,2022; Ijumaa: Juma La 18 La Mwaka

Kutabarukiwa Basilika la Mama Maria
Nyeupe
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Nah. 1: 15; 2:2; 3:1-3, 6-7

Tazama juu ya milima iko miguu yake aletaye habari njema, atangazaye amani. Zishike sikukuu zako, Ee Yuda uziondoe nadhiri zako; kwa maana Yule asiyefaa kitu hatapita kati yako tena kamwe; amekwisha kukatiliwa mbali. Kwa maana Bwana anairudisha fahari ya Yakobo, kama fahari ya Israeli; maana watekao nyara wamewateka, na kuyaharibu matawi ya mizabibu yao.

Ole wake mji wa damu! Umejaa mambo ya uongo na unyang’anyi; mateka hayaondoki. Kelele za mjeledi, kelele za magurudumu yafanyayo kishindo; na farasi wenye kupara-para, na magari ya vita yenye kuruka-ruka; mpanda farasi akipanda, na upanga ukimeta-meta, na mkuki ukimemetuka; na wingi wa waliouawa, na chungu kubwa ya mizoga; mizoga haina mwisho; wanajikwaa juu ya mizoga yao. Nami nitatupa uchafu uchukizao juu yako, kukufanya uwe mchafu, nami nitakufanya kuwa kitu cha kutazamwa kwa dharau. Hata itakuwa, wote wakutazamao watakukimbia, wakisema, “Ninawi umeharibika; ni nani atakayeuhurumia? Nikutafutie wapi wafariji?”

Wimbo Wa Katikati: Kumb. 32: 35-36, 39, 41

 1. Maana siku ya msiba wao imekaribia,
  Na mambo yatakayowapata yatafanya haraka.
  Kwa kuwa Bwana atawaamua watu wake,
  Atawahurumia watumwa wake.

(K) Naua mimi, nahuisha mimi.

 1. Fahamu sasa ya kuwa Mimi, naam, Mimi ndiye.
  Wala hapana Mungu mwingine ila mimi;
  Naua Mimi, nahuisha mimi,
  Nimejeruhi, tena naponya. (K)
 2. Nikiuona upanga wangu wa umeme,
  Mkono wangu ukishika hukumu,
  Nitawatoza kisasi adui zangu,
  Nitawalipa wanaonichukia. (K)

INJILI: Mt. 16:24-28

Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona. Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake; ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.” Amin, nawaambieni, “Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika ufalme wake.”

TAFAKARI
GHARAMA YA UFUASI WETU: Fundisho la Yesu Leo linatualika tutambue namna gani na kwa nini tunatakiwa kuokoa nafsi zetu? Ni rahisi kudhani kuwa mali ya ulimwengu huu ni ya maana zaidi ya vyote na hivi kuzama katika kutumikia mali. Mwingine anaweza kudhani madaraka ya ulimwengu huu ni ya maana zaidi ya vyote na hivi akalewa madaraka na kujiona mmoja kati ya miungu. Tukitaka kuokoa nafsi zetu ni lazima tuitikie kwa vitendo kanuni ya kuwa mfuasi wa Yesu, yaani kujikana mwenyewe, kujitwika msalaba na kumfuata. Yaani, kuwa tayari kuyaacha mali halali ya ulimwengu huu kwa ajili ya kuurithi uzima wa milele; kwa unyenyekevu kuwa tayari kujitoa kwa ajili ya wengine kama alivyofanya Yesu kwa kifo chake msalabani; na kukubali kufundishwa na kuongozwa naye ambaye anatutangulia kama afanyavyo mchungaji mwema. Tunapotafakari juu ya gharama ya kuwa mfuasi wa Yesu tutambue kuwa katika kumfuata Kristo hatuko pekee yetu.

SALA: Ee Mungu, kwa neema unazotujalia utusaidie kuwa jasiri katika kukufuasa wewe huku tukiwa waaminifu katika kanuni za ufuasi wetu. Amina.