Agosti 4,2022; Alhamisi: Juma La 18 La Mwaka

Mt. Yohane Maria Viaaney, Padre
Kumbukumbu
Kijani
SOMO 1: Yer. 31:31-34

“Angalia, siku zinakuja,” asema Bwana, “nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao,” asema Bwana. “Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile,” asema Bwana. “Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, ‘mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao,’ asema Bwana; ‘maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena.”’

Wimbo Wa Katikati: Zab. 51: 10-13, 16-17

 1. Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
  Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
  Usinitenge na uso wako,
  Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.

(K) Ee Mungu, uniumbie moyo safi.

 1. Unirudishie furaha ya wokovu wako;
  Unitegemeze kwa roho ya wepesi.
  Nitawafundisha wakosaji njia zako,
  Na wenye dhambi watarejea kwako. (K)
 2. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,
  Wewe kuridhi sadaka ya kuteketezwa.
  Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika;
  Moyo uliovujika na kupondeka,
  Ee Mungu, hutadharau. (K)

INJILI: Mt. 16:13-23

Yesu alienda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, “Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?” Wakasema, “Wengine hunena u Yohane Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.” Akawaambia, “Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?” Simoni Petro akajibu akasema, “Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Yesu akajibu, akamwambia, “Heri wewe simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali baba yangu aliye mbinguni.” Nami nakuambia, “Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.” Ndipo alipowakataza sana wanafunzi wake wasimwambie mtu yeyote ya kwamba yeye ndiye Kristo. Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuwawa, na siku ya tatu kufufuka. Petro akamchukua akaanza kumkemea, akisema, “Hasha, Bwana, hayo hayatakupata.” Akageuka, akamwambia Petro, “Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”

TAFAKARI
WEWE NDIYE KRISTO, MWANA WA MUNGU ALIYE HAI: Yesu baada ya utume wake wa hadharani, kwanza anataka kupata maoni ya watu juu ya utambulisho wake, na halafu anawageukia na kuwauliza wanafunzi wake swali la msingi juu ya utambulisho huu. Jibu la Petro linadhihirisha kuwa Yesu ni Masiha aliyeahidiwa, ni Mpakwa wa Bwana, na hivi ni zaidi ya Manabii wote. Yesu ni utimilifu wa maaguzi ya Manabii na Mpakwa kwa ajili ya kuleta ukombozi kwa watu wote ili watu wote wapate kuokoka na hivi kuingia kwenye ile heri ya milele tuliyoahidiwa. Kama Petro alivyopata kumuungama Yesu kuwa “Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai”, nasi yatupasa kumuungama Yesu katika maisha yetu huku tukiishi kadiri ya ungamo hilo, yaani kwa kumkiri Yesu kuwa ni Masiha tutambue kuwa Yesu ni Bwana wa Maisha yetu, na hivi tumsikilize na kumfuata yeye ili tuweze hatimaye kuurithi uzima wa milele tunaoutamani.

SALA: Ee Mungu, utujalie ushupavu wa kukukiri wewe kuwa Bwana na Masiha wetu kwa maneno na matendo yetu mema. Amina.