Septemba 3,2022; Jumamosi: Juma La 22 La Mwaka

Mt. Gregori Mkuu, Baba Mt. na Mwalimu wa Kanisa
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: 1Kor. 4: 6-15

Ndugu zangu, mambo hayo nimeyafanya kuwa mfano wa mimi na Apolo kwa ajili yenu, ili kwamba kwa mfano wetu mpate kujifunza kutokupita yale yaliyoandikwa; ili mmoja wenu asijivune kwa ajili ya huyu, kinyume cha mwenziwe. Maana ni nani anayekupambanua na mwingine? Nawe una nini usichokipokea? Lakini iwapo ulipokea wajisifia nini kana kwamba hukupokea? Mmekwisha kushiba, mmekwisha kupata utajiri, mmemiliki pasipo sisi. Naam, laiti mngemiliki, ili sisi nasi tumiliki pamoja nanyi! Maana nadhani ya kuwa Mungu ametutoa sisi mitume mwisho, kama watu waliohukumiwa wauawe; kwa sababu tumekuwa tamasha kwa dunia; kwa malaika na wanadamu. Sisi tu wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini ninyi ni wenye akili katika Kristo; sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu; ninyi mna utukufu, lakini sisi hatupati heshima. Hata saa hii ya sasa, tuna njaa na kiu, tu uchi, twapigwa ngumi, tena hatuna makao; kisha twataabika tukifanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili; tukisingiziwa twasihi; tumefanywa kama takataka za dunia, na tamaa ya vitu vyote hata sasa. Siyaandiki hayo ili kuwatahayarisha; bali kuwaonya kama watoto niwapendao. Kwa kuwa ijapokuwa mna waalimu kumi elfu katika Kristo, walakini hamna baba wengi. Maana mimi ndimi niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa njia ya injili.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 145: 17- 21

 1. Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
  Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.
  Bwana yu karibu na wote wamwitao,
  Wote wamwitao kwa uaminifu.

K: Bwana yu karibu na wote wamwitao.

 1. Atawafanyia wamchao matakwa yao,
  Naye atakisikia kilio chao na kuwaokoa.
  Bwana huwahifadhi wote wampendao,
  Na wote wasio haki atawaangamiza. (K)
 2. Kinywa changu kitazinena sifa za Bwana;
  Wote wenye mwili na walihimidi jina lake takatifu
  Milele na milele. (K)

INJILI: Lk. 6:1-5

Ilikuwa siku ya sabato moja Yesu alikuwa akipita katika mashamba, wanafunzi wake wakawa wakivunja masuke na kuyala, wakiyapukusa-pukusa mikononi mwao. Basi baadhi ya Mafarisayo wakawaambia, “Mbona mnafanya lisilo halali siku ya sabato?” Yesu akawajibu akawaambia, “Hamkulisoma hata hilo alilolifanya Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wale aliokuwa nao?” Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaitwaa mikate ile ya Wonyesho, akaila akawapa na hao wenziwe, ambayo si halali kuila ila kwa makuhani pekee yao. Akawaambia, “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.”

TAFAKRI
TUTENDE MEMA KILA WAKATI: Neno la Mungu leo linatufundisha kutenda mema kila wakati. Uwepo wa sheria mbalimbali zinazohusu dini yetu zinapaswa kutusaidia kuwa karibu zaidi na Mungu. Sheria ya sabato ilikusudiwa pia kuwasaidia Taifa la Mungu kupata muda wa kutenda mema na haikukusudiwa kuwa mzigo. Tujifunze kutenda mema kwa kadiri ya hitaji la sheria na siyo kujikita kwenye maneno ya sheria. Tukishika maneno ya sheria tunaweza kujikuta tunaenda mbali na Mungu badala ya kuwa karibu naye. Sheria yoyote huwa nzuri na hupata maana zaidi inaposukumwa na upendo wa Mungu. Sheria ya sabato ilisukumwa na upendo wa Mungu ili watu wapate muda wa kumwabudu. Sheria hiyo inapotafsiriwa vibaya inapoteza kusudio la Mungu. Tusiogope kutenda mema, tusiogope kukosea katika jitihada za kutenda mema. Yesu amesahihisha uelewa hasi wa wale waliojikita katika maneno ya sheria kwa kunukuu Maandiko Matakatifu akikumbusha namna Daudi na wenzake walivyokula mikate ya wonyesho, ili kutuliza njaa.

SALA: Ee Mungu, naomba moyo wa kutenda mema daima.Amina.