Agosti 3,2022; Jumatano: Juma La 18 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Yer. 31:1-7

“Wakati huo,” asema Bwana, “Nitakuwa Mungu wa jamaa zote za Israeli, nao watakuwa watu wangu.” Bwana asema hivi, “Watu wale walioachwa na upanga walipata neema jangwani; yaani, Israeli, hapo nilipokwenda kumstarehesha.” Bwana alinitokea zamani, akisema, “Naam, nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu. Mara ya pili nitakujenga, nawe utajengwa. Ee bikira wa Israeli, mara ya pili utapambwa kwa matari yako, nawe utatokea katika michezo yao wanaofurahi. Mara ya pili utapanda mizabibu juu ya milima ya Samaria; wapanzi watapanda, nao watayafurahia matunda yake. Maana kutakuwa siku moja, ambayo walinzi watalia juu ya vilima vya Efraimu, “Inukeni, tukaende Sayuni, kwa Bwana, Mungu wetu.” Maana Bwana asema hivi, “Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mkampigie kelele mkuu wa mataifa, tangazeni, sifuni, mkaseme, ‘Ee Bwana, uwaokoe watu wako mabaki ya Israeli.”’

Wimbo Wa Katikati: Yer. 31:10-13

 1. Lisikieni neno la Bwana,
  enyi mataifa, litangazeni visiwani mbali,
  mkaseme, “Aliyemtawanya Israeli atamkusnya,
  na kumlinda, kama mchungaji alindavyo kundi lake.”
  Kwa maana Bwana amemweka huru Yakobo,
  amemkomboa mkononi mwake
  aliyekuwa Hodari kuliko yeye.

(K) Bwana atatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.

 1. Nao watakuja, na kuimba katika mlima Sayuni,
  wataukimbilia wema wa Bwana, nafaka, na divai;
  na mafuta, na wachanga wa kondoo na wa ng’ombe;
  na roho zao zitakuwa kama bustani iliyotiwa maji;
  wala hawatauzunika tena kabisa. (K)
 2. Ndipo bikira atafurahi katika kucheza,
  na vijana na wazee pamoja;
  maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha,
  nami nitawafariji,
  na kuwafurahisha waache huzuni zao. (K)

INJILI: Mt. 15:21-28

Yesu aliondoka Genezareti akaenda kando pande za Tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, “Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo.” Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, “Mwache aende zake; Kwa maana anapiga kelele nyuma yetu.” Akajibu, akasema, “Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.” Naye akaja akamsujudia, akisema, “Bwana unisaidie.” Akajibu, akasema, “Si vema kukitwaa chakula cha wototo na kuwatupia mbwa.” Akasema, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao.” Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, “Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo.” Akapona binti yake tangu saa ile.

TAFAKARI
NGUVU YA SALA NA IMANI: Mwanamke Mkananayo kwa kuwa ni mtu wa Mataifa anamwita Yesu kwa mbali akiheshimu sheria za mahusiano kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi. Hitaji lake ni halisi na la lazima ndio maana licha ya kikwazo cha kimahusiano ya kikabila alimwendea Yesu, japo kwa mbali. Hitaji na imani yake kwa Yesu vinaonekana kwa namna ya kupeleka ombi lake (kupaza sauti) na majibu yake kwa maneno makali ya Yesu. Mwanamke Mkananayo hakuvunjika moyo wala hakukata tamaa, aliendelea kuomba kwa imani. Tena mwanamke huyu Mkananayo anatenda hayo yote kwa ajili ya binti yake. Akitufundisha juu ya sala na maombi kwa ajili ya mahitaji ya wengine hasa wenye shida na mahitaji mbalimbali. Imani na udumifu katika kuomba kumemletea mapato mazuri mwanamke huyu Mkananayo. Binti yake anaponywa toka muda Yesu anapotamka, “Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo.” Mama huyu awe mfano kwetu wa kusali kwa imani na bila kuchoka na kuwaombea wengine.

SALA: Ee Mungu, uzidi kutujalia neema zako ili tuweze kudumu katika sala bila kukata tamaa. Amina.