Agosti 2,2022 Jumanne: Juma La 18 La Mwaka

Mt. Eusebi wa Verselli, Askofu
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Yer. 30:1-2, 12-15, 18-22

Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema, “Bwana Mungu wa Israeli,” asema hivi, ya kwamba, uyaandike kitabuni maneno hayo niliyokuambia. Maana Bwana asema hivi, “Maumivu yako hayaponyeki, na jeraha yako ni kubwa. Hapana mtu wa kukutetea; kwa jeraha yako huna dawa ziponyazo. Wote wakupendao wamekusahau; hawakutafuti; maana nimekujeruhi kwa jeraha ya adui, kwa adhabu ya mtu mkatili; kwa sababu ya ukubwa wa uovu wako, kwa sababu ya dhambi zako zilikuwa zimeongezeka. Mbona unalilia maumivu yako? Hayaponyeki maumivu yako; kwa sababu ya ukubwa wa uovu wako, kwa sababu ya dhambi zako zimeongezeka, nimekutenda haya.” Bwana asema hivi, “Tazama, nitarudisha tena hema za Yokobo zilizohamishwa, na kuyahurumia makosa yake; nao mji huo utajengwa juu ya magofu yake wenyewe, nalo jumba litakaliwa, kama ilivyokuwa desturi yake. Tena kwao itasikiwa shukrani, na sauti yao wachangamkao; nami nitawazidisha, wala hawatakuwa wachache; tena nitawatukuza, wala hawatakuwa wanyonge. Watoto wao nao watakuwa kama zamani, na kusanyiko lao litathibitika mbele zangu, nami nitawaadhibu wote wawaoneao. Na mkuu wao atakuwa mtu wa kwao wenyewe, naye mwenye kuwatawala atakuwa mtu wa jamaa yao; nami nitamkaribisha, naye atanikaribia; maana ni nani aliye na moyo wa kuthubutu kunikaribia?” Asema Bwana. “Nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 102:15-20, 28, 21-22

 1. Kisha mataifa wataliogopa jina la Bwana,
  Na wafalme wote wa dunia utukufu wako;
  Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni,
  Atakapoonekana katika utukufu wake,
  Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa,
  Asiyadharau maombi yao.

(K) Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni,
atakapoonekana katika utukufu wake.

 1. Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo,
  Na watu watakaoumbwa watamsifu Bwana.
  Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu,
  Toka mbinguni Bwana ameiangalia nchi,
  Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa,
  Na kuwafungua walioandikiwa kufa. (K)
 2. Wana wa watumishi wako watakaa,
  Na wazao wao wataimarishwa mbele zako.
  Watu walitangaze jina la Bwana katika Sayuni,
  Na sifa zake katika Yerusalemu,
  Pindi mataifa watakapokusanyika pamoja,
  Falme nazo ili kumtumikia Bwana. (K)

INJILI: Mt. 15: 1-2, 10-14 au (Mt. 14:22-36)

(Somo hili linasomwa kwa sababu Mt. 14:22-36 lilisomwa Jumatatu)

Mafarisayo na waandishi toka Yerusalemu walipomwendea Yesu wakisema, “Mbona wanafunzi wako huyahalifu mapokeo ya wazee, kwa maana hawanawi mikono wakati walapo chakula.” Akawaita makutano akawaambia, “Sikilizeni, mfahamu; Sicho kiingiacho kinywani kimtiacho mtu unajisi; bali kitokacho kinywani ndicho kimtiacho mtu unajisi.” Ndipo wanafunzi wake walipomwendea, wakamwambia, “Wajua ya kuwa Mafarisayo walipolisikia neno lile walichukizwa?” Akajibu, akasema, “Kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang’olewa. Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili.”

TAFAKARI
TUSAFISHE MIOYO YETU: Mashtaka ya Mafarisayo na Waandishi waliyoyapeleka kwa Yesu dhidi ya Wanafunzi wake yanaweka mkazo juu ya kushika sheria za usafi wa nje. Kutokana na muono huu wa Mafarisayo na Waandishi, Yesu anawaona hawa kuwa ni ‘viongozi vipofu wa vipofu’. Maana yake Mafarisayo na Waandishi hawana elimu au ujuzi juu ya sheria za Mungu, hivyo kwa mafundisho yao ni wapotoshaji wa ukweli. Jibu la Yesu kwa Mafarisayo na Waandishi linasisitiza umuhimu wa kwanza wa kushika sheria za usafi wa ndani ya mtu. Yesu kwa jibu lake anaonyesha kuwa unajisi hauhusiani na mambo ya nje nje kama kushika sabato, sheria za kuosha vyombo au mambo yahusuyo vyakula, isipokuwa usafi wa ndani, usafi wa moyo. Kwani ndani ya moyo wa mtu ndimo ambamo huanzia dhambi amabazo huonekana nje kwa maneno na matendo ya mtu. Ukweli huu unaelezwa kinaganaga na Nabii Yeremia katika kitabu chake (17:9–10). Tunaalikwa kuwa na usafi wa ndani kwa kusafisha mioyo yetu.

SALA: Ee Mungu, utuepushe na dhambi za mawazo. Uijaze mioyo yetu mawazo mema. Amina.