Julai 31,2022; Jmapili: Jumapili Ya 18 Ya Mwaka

SOMO 1: Mhu. 1:2, 2:21-23

SOMO 2: Kol. 3:1-5, 9-11

Mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu. Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu. Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu. Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake; mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba. Hapo hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote.

SHANGILIO: Efe. 1:17, 18
Aleluya, aleluya,
Ewe Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo,
Uijalie nuru macho ya mioyo yetu,
Ili tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo.
Aleluya.

INJILI: Lk. 12:13-21

Mtu mmoja katika mkutano alimwambia, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu.” Akamwambia, “Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu?” Akawaambia, “Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.” Akawaambia mithali, akisema, “Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, ‘Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu?’” Akasema, “Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, ‘Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi.’” Lakini Mungu akamwambia, “Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?” Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.

TAFAKARI
TUITAWALE MALI SIYO MALI ITUTAWALE SISI: wazo hili linajitokeza wazi wazi katika mfano wa tajiri aliyekuwa akipanga namna ya “kufaidi mazao yake”, kwa lugha za vijana “kula bata”. Wazo hili linajitokeza pia katika masomo yanayoisindikiza Injili.
Mfano tuliosomewa, Yesu halaani shughuli za kujitegemea kama kulima na wala hayalaani mafanikio kama ya kupata mavuno manono. Suala linalokusudiwa kuwekwa wazi ni ujinga wa kuweka moyo kwenye mali na kumsahau Mungu. Laiti tajiri yule angeyapokea mavuno yake huku akimtia Mungu katika hesabu zake, asingeangamia.
Kati ya Wayahudi walikuwapo wakulima mbalimbali kama wa nafaka, tende, tini na zeituni. Kama wakulima wowote wale mavuno manono hukosha sana mioyo yao. Kufurahi kwa kupata kitu si dhambi pia. Kosa la tajiri ilikuwa kuweka furaha yake kwenye mipaka ya mali yake tu. Hakuwa mtawala wa mali zake maana kinachotawaliwa lazima kiwe chini ya mtawala. Mali ikitawala inakuwa juu ya mtu. Inapotokea hivyo yanatimia yale aliyoonya Yesu (Mt 6:24) ndiyo kujipatia mabwana wawili ambao si rahisi kuwatumikia wote kwa upendo wa kiwango sana.
Somo la kwanza linasikitikia mkasa wa mali kwamba mtu anaweza kujituma sana kuitafuta lakini kwa kuwa hana uwezo wa kutawala muda ujao, akifa mali hiyo inaweza kuangukia mikononi mwa mpumbavu fulani tu. Jambo hili mhubiri analiona kuwa ubatili wa kusikitisha mno.
Somo la pili linatoa mwongozo wa maisha yenye mustakabali wa kweli. Linasema ni mtu kuishi akiyachuchumia mambo ya juu Kristo aliko. Ni kuachana na kuwekeza moyo hapa duniani kwa kujibari na maovu ambayo yanammalizia mtu katika maangamizi hapa duniani. Ni kwa sababu hiyo, somo linawaasa Wakristo wote kwa vile wamefufuliwa pamoja na Kristo, wayatafute mambo adhimu yaliyo juu, Kristo aliko, akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Linawaomba watu wayafikirie mambo yaliyo juu, siyo ya hapa chini. Kwa maneno mengine, kwa kufanyika watu wapya, uhai wao umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu nao watumaini kufunuliwa pamoja naye katika utukufu. Mwishowe somo linawaelekeza likisema kusudi wasikose shabaha ya kutamalaki pamoja na Yesu Kristo mbinguni, wana kazi ya kuvifisha viungo vyao vilivyo katika nchi wakizikabili vilivyo dhambi za uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, inayomaanisha ibada ya sanamu. Zaidi ya hayo, wasiambiane uongo. Shime tuyatendee haki.
Kwa kumalizia tusisitize tena wanadamu tujitahidi kutawala mali zetu, zisije zikatuponza. Kifupi, wanadamu tujitahidi kuwa mabwana wa vitu na siyo vitu vituzukie mabwana zetu. Tukumbuke katika kitabu cha Mwanzo (Mw 1:26-28), Mungu alitupa nguvu ya kutawala viumbe wake wote.

SALA: Ee Mungu Mwenyezi, umetuumba na kutukabidhi ulimwengu uliojaa mema mengi. Tusaidie hata siku moja mali hizo zisigeuke mabwana zetu kwani Bwana wetu wapaswa kuwa wewe peke yako. Amina.