Julai 30,2022; Jumamosi: Juma La 17 La Mwaka

Mt. Petro Krisologi, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Yer. 26:11-16, 24

Makuhani na manabii, waliwaambia wakuu na watu wote, wakisema, “Mtu huyu amestahili kufa, kwa sababu ametabiri juu ya mji huu, kama mlivyosikia kwa masikio yenu.” Ndipo Yeremia akawaambia wakuu wote na watu wote, akisema, “Bwana ndiye aliyenituma kuitabiri juu ya nyumba hii, na juu ya mji huu, maneno hayo yote mliyoyasikia. Basi sasa, tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, mkaisikilize sauti ya Bwana, Mungu wenu; naye Bwana atayaghairi mabaya aliyoyanena juu yenu. Lakini kwangu mimi, tazama, mimi nipo hapa mikononi mwenu; nitendeni myaonayo kuwa mema na haki mbele ya macho yenu. Lakini jueni yakini ya kuwa, mkiniua, mtajiletea juu yenu damu isiyo na hatia; itakuwa juu yenu, na juu ya mji huu, na juu ya wenyeji wake; kwa maana ni kweli Bwana amenituma kwenu, kuwaambieni yote mliyoyasikia.” Ndipo wakuu na watu wote wakawaambia makuhani, na manabii, wakisema, “Mtu huyu hastahili kuuawa; kwa maana amesema nasi katika jina la Bwana, Mungu wetu.” Mkono wa Ahikamu, mwana wa Shafani, ulikuwa pamoja na Yeremia, wasimtie katika mikono ya watu auawe.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 69: 14-15, 29-30, 32

 1. Mungu na atufadhili na kutubariki,
  Na kutuangazia uso wake.
  Njia yake ijulikane duniani,
  Wokovu wake katikati ya mataifa yote.

(K) Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, Ee Mungu.

 1. Mataifa na washangilie,
  Naam, waimbe kwa furaha,
  Maana kwa haki utawahukumu watu,
  Na kuwaongoza mataifa walioko duniani.(K)
 2. Nchi imetoa mazao yake;
  Mungu, Mungu wetu, ametubariki.
  Mungu atatubariki sisi;
  Miisho yote ya dunia itamcha Yeye.(K)

INJILI: Mt.14:1-12

Mfalme Herode alisikia habari za Yesu, akawaambia watumishi wake, “Huyo ndiye Yohane Mbatizaji; amefufuka katika wafu; na kwa hiyo nguvu hizo zinatenda kazi ndani yake.” Maana Herode alikuwa amemkamata Yohane, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye. Kwa sababu Yohane alimwambia, “Si halali kwako kuwa naye.” Naye alipotaka kumwua, aliwaogopa watu, maana walimwona Yohane kuwa nabii. Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode. Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lo lote atakaloliomba. Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, “Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohane Mbatizaji.” Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru apewe; akatuma mtu, akamkata kichwa Yohane mle gerezani. Kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule kijana; akakichukua kwa mamaye. Wanafunzi wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha Yesu habari.

TAFAKARI
TUUPOKEE UKWELI NA KUBADILIKA: Nabii Yeremia alipotoa utabiri juu ya kuangamia kwa miji yote ya Yuda, hakuogopa lolote au yeyote. Kwake yeye ukweli kutoka kwa Mungu lazima uwafikie ili uwaponye. Kwa bahati njema, kwa utetezi alioutoa Yeremia na kwa mikono ya Ahikamu, mwana wa Shafani, aliweza kuokolewa na nia mbaya ya makuhani na manabii waliotaka kumuua. Mambo hayakuwa hivi kwa Yohane Mbatizaji ambaye naye kwa kuutetea ukweli na haki, alitiwa kifungoni. Alimweleza Mfalme Herode juu ya tendo lake ovu la kumchukua mke wa ndugu yake, Filipo. Dhambi hii ya Herode haiishii kumuweka kifungoni Yohane Mbatizaji bali inakua na kuzaa mauti. Mfalme Herode kutokana na kumwahidi mwanaye, anaamuru Yohane Mbatizaji akatwe kichwa. Sisi tunaupokeaje ukweli katika maisha yetu? Mara ngapi tumeingia katika ugomvi na vita kati yetu kwa kuwa tu tumeacha kuupokea ukweli. Tukitaka kweli kuwa wana wapendwa wa Mungu, tuwe tayari kuupokea ukweli na utusaidie kubadilika. Hata tukiharibu sifa njema za wale wanaotuambia ukweli, hatutaweza kuuzima ukweli kamwe.

SALA: Tunakuomba utuondolee hofu ya kusema ukweli ili tuweze kuuponya ulimwengu wetu, Amina.