Julai 29;2022; Ijumaa: Juma La 17 La Mwaka

Mt. Marta
Kumbukumbu
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Yer. 26:1-9

Mwanzo wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili lilitoka kwa Bwana, kusema, Bwana asema hivi, “Simama katika uwanja wa nyumba ya Bwana, useme na miji yote ya Yuda, wajao ili kuabudu katika nyumba ya Bwana; sema nao maneno yote ninayokuamuru kuwaambia, usizuie hata neno moja. Labda watasikia, na kughairi na kuacha kila mtu njia yake mbaya; ili niyaghairi mabaya niliyokusudia kuwatenda, kwa sababu ya uovu wa matendo yao.” Nawe utawaambia, Bwana asema hivi, “Kama hamtaki kunisikia, kwenda katika sheria yangu, niliyoiweka mbele yenu, kuyasikiliza maneno ya watumishi wangu, manabii, ninaowatuma kwenu, naam, nikiondoka mapema na kuwatuma; lakini ninyi hamkuwasikiliza; basi, nitafanya nyumba hii kuwa kama Shilo, na mji huu nitaufanya kuwa laana kwa taifa zote za dunia.” Na makuhani, na manabii, na watu wote, wakamsikia Yeremia, hapo aliposema maneno haya katika nyumba ya Bwana. Ikawa, Yeremia alipokuwa amekwisha kusema maneno yote ya Bwana aliyomwamuru kuwaambia watu wote, ndipo hao makuhani, na manabii, na watu wote, wakamkamata, wakisema, “Bila shaka utakufa. Kwa nini umetabiri kwa jina la Bwana, ukisema, ‘nyumba hii itakuwa kama Shilo, na mji huu utakuwa ukiwa, hautakaliwa na mtu?’” Watu wote wakamkusanyikia Yeremia katika nyumba ya Bwana.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 69:4, 7-9, 13

 1. Wanaonichukia bure ni wengi
  Kuliko nywele za kichwa change.
  Watakao kunikatilia mbali wamekuwa Hodari,
  Adui zangukwa sababu isiyo kweli.
  Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu
  Vitu nisivyovichukua.

(K) Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, ee Bwana.

 1. Maana kwa ajili yako nimestahimili laumu,
  Fedheha imenifunika uso wangu.
  Na msikwao kwa wana wa mama yangu.
  Maana wivu wa nyumba yako umenila,
  Na laumu zao wanaokulaumu zimenipata. (K)
 2. Nami maombi yangu nakuomba Wewe, Bwana,
  Wakati ukupendezao; Ee Mungu,
  Kwa wingi wa fadhila zako unjibu,
  Katika kweli ya wokovu wako. (K)

INJILI: Mt. 13: 54-58

Yesu alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, “Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si mwana wa Seremala? Mamaye si yeye aitwae Mariamu? na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote?” Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, “Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe.” Wala hakufanya miujiza mingi huko kwa sababu ya kutokuamini kwao.

TAFAKARI
NABII HAKOSI KUPATA HESHIMA, ISIPOKUWA KATIKA NCHI YAKE: kazi kubwa wanayoipata wahubiri au mapadre ni kupeleka Neno la Mungu katika mazingira waliyozaliwa au kukulia. Hii mara nyingi inatokana na mmoja kufahamika katika mazingira hayo. Hivyo, badala ya watu kuyapokea maneno wanayoambiwa, wao wanayafananisha maneno hayo ma maisha ya msemaji, familia yake na hata mapungufu yake. Leo tunamuona Yesu anapata shida kupokelewa katika mji wake. Mafundisho yake yanawagusa wote na hata wanaushangaa uwezo wake mkubwa. Lakini wanaishia kusema. “Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si ….? Mamaye si ….?” Wanaacha kulipokea Neno na kuanza kumjadili mleta Neno, hasa mapungufu yake. Nabii Yeremia katika somo la kwanza anapata ugumu wa kupokelewa na wanafikira kumuua kwa kuwa anawaeleza ukweli. Kamwe tusikose kulisikiza Neno tukaanza kumjadili mleta Neno. Kamwe tusiwe kama waliochomwa na Neno wakawageukia wajumbe wa Mungu (Yeremia na Yesu), kutaka kuwaangamiza. Tuyapokee maonyo na maelekezo na tuwe tayari kuwapokea wajumbe wa Mungu.

SALA: Ee Mungu, Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga wa kuniongoza, Amina.