Julai 28,2022; Alhamisi: Juma La 17 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Yer. 18:1-6

Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema, “Ondoka, ukashuke mpaka nyumba ya mfinyanzi, na huko nitakusikizisha maneno yangu. Basi nikashuka mpaka nyumba ya mfinyanzi, na tazama, alikuwa akifanya kazi yake kwa magurudumu. Na chombo kile alichokuwa akikifinyanga, kilipoharibika mkononi mwake yule mfinyanzi, alikifanyiza tena kuwa chombo kingine, kama alivyoona vyema yule mfinyanzi kukifanya.” Ndipo neno la Bwana likanijia, kusema, “Ee nyumba ya Israeli, je! Siwezi mimi kuwatendea ninyi vile vile kama mfinyanzi huyu alivyotenda?” Asema Bwana. “Angalieni, kama udongo ulivyo katika mkono wa mfinyanzi, ndivyo mlivyo katika mkono wangu, Ee nyumba ya Israeli.”

Wimbo Wa Katikati: Zab 146: 1-5

 1. Ee nafsi yangu, umsifu Bwana,
  Nitamsifu Bwana muda nitakaoishi,
  Nitamwimbia Mungu ningali ni hai.

(K) Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake.

 1. Msiwatumainie wakuu,
  Wala binadamu ambaye hakuna wokovu kwake.
  Pumzi yake hutoka, huurudia udongo wake,
  Siku hiyo mawazo yake yatapotea. (K)
 2. Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake,
  na tumaini lake ni kwa Bwana, Mungu wake.
  Aliyezifanya mbingu nan chi,
  bahari na vitu vyote vinavyoonekana. (K)

INJILI: Mt. 13:47-53

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya wa kila namna; hata lilipojaa, walilivuta Pwani, wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa. Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; Malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.” Yesu aliwauliza, “Mmeyafahamu hayo yote?” Wakamwambia, “Naam.” Akawaambia, “Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.” Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake.

TAFAKARI
HUJAFA HUJAUMBIKA: Mfinyazi tunayemsikia katika somo la kwanza anatukumbusha namna sisi binadamu tunavyoendelea kufinyangwa na kuundwa upya na Mungu kila siku ya maisha yetu. Namna Mungu alivyotuumba tumboni mwa mama zetu na anavyoendelea kutufinyanga hadi sasa, ni siri yake na uweza wake. Nabii Yeremia anaeleza wazi maneno ya Mungu mwenyewe akisema “Angalieni, kama udongo ulivyo katika mkono wa mfinyanzi, ndivyo mlivyo katika mkono wangu, Ee nyumba ya Israeli”. Mara kwa mara tunapomkosea au kutenda kinyume na mapenzi yake, kama udongo anatufinyanga tena ili tuwe watu wema na wenye kumpendeza. Ni vizuri tukajiulize, mara ngapi tumefinyangwa na bado tumerudia katika hali ya kutompendeza? Tunataka tufinyangwe mara ngapi ili tuendane na matakwa yake? Tukidumu katika ukaidi wetu, si haba kutopata anayoyaeleza Yesu leo juu ya mfano wa juya lililotupwa baharini, na lilipopelekwa pwani, ndipo samaki wema wakawekwa vyomboni na wabaya wakatupwa. Tusisubiri juya litupitie na baadaye tukatupwe.

SALA: Ee Mungu, twakuomba uendelee kutuumba kwa Neno lako, Amina.