Julai 27,2022; Jumatano: Juma La 17 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Yer. 15:10, 16-21

Ole wangu, mama yangu, kwa kuwa umenizaa mtu wa kuteta, na mtu wa kushindana na dunia yote! Mimi sikukopesha kwa riba, wala watu hawakunikopesha kwa riba; lakini kila mmoja wao hunilaani. Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, ee bwana, Mungu wa majeshi. Sikuketi katika mkutano wao wanaojifurahisha, wala sikufurahi; naliketi peke yangu kwa sababu ya mkono wako; kwa maana umenijaza ghadhabu. Mbona maumivu yangu ni ya daima, na jeraha yangu haina dawa, inakataa kuponywa? Je! Yamkini wewe utakuwa kwangu kama kijito kidanganyacho, na kama maji yasiyodumu? Kwa sababu hiyo Bwana asema hivi, “Ukirudi, ndipo mimi nitakapokurejeza, upate kusimama mbele zangu; nawe ukitoa kilicho cha thamani katika kilicho kibovu, utakuwa kama kinywa changu; nao watakurudia wewe, bali hutawarudia wao. Nami nitakufanya kuwa kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na kukuponya, asema Bwana. Nami nitakuokoa na mkono wa watu wabaya, nami nitakukomboa katika mkono wao wenye kutisha.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 59:1-4, 9-10, 16-17

 1. Ee Mungu wangu, uniponye na adui zangu,
  Uniinue juu yao wanaoshindana nami.
  Uniponye nao wafanyao maovu,
  Uniokoe na watu wa damu.

(K) Bwana alikuwa ngome yangu siku ya shida yangu.

 1. Kwa maana wanaiotea nafsi yangu;
  Wenye nguvu wamekusanyikia;
  Ee Bwana, si kwa kosa langu;
  Bila kosa langu huenda mbio, hujiweka tawari;
  Uamke uonane nami, na kutazama. (K)
 2. Ee nguvu zangu,nitakungoja wangu,
  Maana Mungu ndiye aliye ngome yangu.
  Mungu wa Fadhili zangu atanitangulia,
  Mungu atanijalia kuwatazama adui zangu. (K)
 3. Nami nitaziimba nguvu zako asubuhi,
  Nitaziimba Fadhili zako kwa furaha.
  Kwa kuwa ndiwe uliyekuwa ngome yangu,
  Na makimbilio siku ya shida yangu. (K)

INJILI: Mt. 13:44-46

Yesu aliwaambia makutano mifano, “Ufalme wa Mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile. Tena Ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri; naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua.”

TAFAKARI
UFUASI WETU KWA KRISTO NI LULU YA THAMANI KUBWA: Tumezoea kuona na kusikia habari za watu wenye vitu vya thamani namna walivyotolea jasho kuvipata. Kama miaka miwili iliyopita, tulisikia habari ya mchimbaji mmoja wa madini ya “tanzanite” alivyopata mawe makubwa na ya thamani kubwa, aliyachimba chini sana na ilikuwa kazi ngumu na ya kuchosha. Ukatoliki wetu endapo tunauweka katika mizani ya thamani, hakuna cha kuulinganisha nao, na hasa tukiutafakari Ukatoliki huu/ufuasi wetu kwa Kristo kama njia pekee ya mmoja kurithi mbingu. Yawezekana wengine tusiione thamani hii kubwa ya ufuasi wetu labda kwa kuwa hatuuhangaikii sana kama alivyohangaika yule mchimbaji. Tusisahau kuwa thamani yake imetokana na kifo cha Yesu msalabani, huu ndio mtaji wetu. Sasa, iwe tumeutolea jasho jingi au dogo, tufahamu tu kuwa ufuasi wetu ni lulu yenye thamani. Ni hazina ambayo kila mmoja wetu anaweza kuimiliki kwa kutumia utayari wetu wa kumfuasa Kristo kwa kuishi maisha yampendezayo Mungu. Tuyapokee maneno ya Mungu yanayotuletea furaha.
SALA: Mungu Mwema, Wewe Ndiye Yote Katika Maisha Yetu, Amina.