Julai 26,2022; Jumanne: Juma La 17 La Mwaka

Wat. Joakim na Anna, Wazazi wa Bikira Maria
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Yer. 14:17-22

Macho yangu na yatiririke machozi, usiku na mchana; wala yasikome; kwa maana bikira, binti ya watu wangu, amevunjika mavunjiko makuu, kwa jeraha isiyoponyeka. Nikitoka kwenda shambani, tazama, wako huko waliouawa kwa upanga! Na nikiingia mjini, tazama, wamo humo wanaougua kwa sababu ya njaa! Maana nabii na kuhani, wote wawili, huenda huko na huko katika nchi, wala hawana maarifa. Je! Umemkataa Yuda kabisa? Roho yako imeichukia sayuni? Mbona umetupiga, tusiwe na dawa ya kutuponya? Tulitazamia amani, lakini hayakuja mema yo yote; tulitazamia wakati wa kupona, na tazama, kufadhaika tu! Ee bwana, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba zetu; maana tumekutenda dhambi. Usituchukie, kwa ajili ya jina lako; usikifedheheshe kiti cha enzi cha utukufu wako; kumbuka, usilivunje agano ulilofanya nasi. Je! Katika vitu vya ubatili vya mataifa, kiko kitu kiwezacho kuleta mvua? Je! Mbingu zaweza kutoa manyunyu? Je! Si wewe, ee Bwana, Mungu wetu? Kwa sababu hiyo tutakungoja; kwa kuwa wewe umevifanya vitu hivi vyote.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 79:8-9, 11, 13

 1. Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu,
  Rehema zako zije kutulaki kama hima.
  Kwa maana tumedhilika sana.

(K) Kwa ajili ya utukufu wa jina lako, utusaidie, ee Bwana

 1. Ee Mungu wa wokovu wetu utusaidie,
  Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
  Utuokoe, utughofir dhambi zetu,
  Kwa ajili ya jina lako. (K)
 2. Kuungua kwake aliyefungwa na kuingia mbele zako,
  Kwa kadiri ya uwezo wa mkono wako
  Uwahifadhi wana wa mauti.
  Na sisi tulio watu wako, na kondoo za malisho yako,
  Tutashukuru milele;
  Tutazisimulia sifa zako kizazi kwa kizazi. (K)

INJILI: Mt. 13:36-43

Yesu aliwaaga makutano, akaingia nyumbani; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, “Tufafanulie mfano wa magugu ya kondeni.” Akajibu, akasema, “Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu; lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu; yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika. Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watakapong’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio na asikie.”

TAFAKARI
TUTAVUNA TULICHOPANDA: Mkulima yeyote hutegemea kuvuna kile alichokipanda katika shamba lake. Ili kupata mavuno mazuri zaidi, lazima katika kilimo chake atumie ushauri wa wataalamu na kufanya kila shughuli ya shamba kwa wakati. Leo Yesu anapotoa ufafanuzi wa mfano wake wa magugu ya kondeni, ni nzuri kwetu kuona namna gani sisi kama wana wa Mungu tunatumia neema na baraka za Mwenyezi Mungu katika kuhakikisha kuwa tunajiandaa vema kwa ajili ya maisha ya umilele mbinguni. Tukikumbuka kuwa hapa duniani tu wapitaji tu na namna tunavyoishi vizuri sasa ndivyo tunavyozidi kuusogelea ufalme wa Baba, basi tukumbuke wajibu wetu wa kutumia vizuri misaada mbalimbali ambayo Mungu ametupatia, kama sakramenti ya upatanisho. Nabii Yeremia anaeleza wazi hili anapotuambia “Ee bwana, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba zetu; maana tumekutenda dhambi”. Hivyo jukumu la kutubu ni la muhimu. Tusimpe nafasi Ibilisi aliye mwovu akaendelea kupanda magugu katika mioyo yetu.

SALA: Tu wakosefu Baba Mungu, tunaomba msamaha wako ili tukurudie Wewe, Amina.