Julai 24,2022; Jumapili: Jumapili Ya 17 Ya Mwaka

SOMO 1: Mwa. 18:20-32

Bwana alisema, “Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana. Basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua.” Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za Bwana. Ibrahimu akakaribia, akasema, “Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu? Huenda wakawapo wenye haki hamsini katika mji, utaharibu, wala hutauacha mji kwa ajili ya hao hamsini wenye haki waliomo? Hasha, usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha; Mhukumu ulimwengu wote asitende haki?” Bwana akasema, “Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao.” Ibrahimu akajibu, akasema, “Basi, nimeshika kusema na Bwana, nami ni mavumbi na majivu tu. Huenda wakapunguka watano katika wale hamsini wenye haki, Je! Utaharibu mji wote kwa kupungua watano?” Akasema, “Sitauharibu, nikiona humo arobaini na watano.” Akazidi tena kusema naye, akinena, “Huenda wakaonekana humo arobaini?” Akasema, “Sitafanya kwa ajili ya hao arobaini.” Akasema, “Bwana asiwe na hasira, nami nitasema, Huenda wakaonekana huko thelathini?” Akasema, “Sitafanya, nikiona humo thelathini.” Akasema, “Tazama, nimeshika kusema na Bwana, huenda wakaonekana huko ishirini?” Akasema, “Sitaharibu kwa ajili ya hao ishirini.” Akasema, “Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi?” Akasema, “Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 138:1-3, 6-9

 1. Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,
  Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
  Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu,

(K) Siku ile niliyokuita uliniitikia,
Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu.

 1. Nitalishukuru jina lako,
  Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
  Kwa maana umekuza ahadi yako,
  Kuliko jina lako lote.
  Siku ile niliyokuita uliniitikia,
  Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. (K)
 2. Ingawa Bwana yuko juu, amwona mnyenyekevu,
  Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali.
  Nijapokwenda kati ya shida atanihuisha,
  Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu. (K)
 3. Na mkono wako wa kuume utaniokoa.
  Bwana atanitimiliza mambo yangu;
  Ee Bwana, fadhili zako ni za milele;
  Usiziache kazi za mikono yako. (K)

SOMO 2: Kol. 2:12-14

Mkazikwa pamoja na Kristo katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu. Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani.

SHANGILIO: Yn. 14:23

Mtu akinipenda, atashika neno langu, na Baba yangu atampenda;
Nasi tutakuja kwake.
Aleluya.

INJILI: Lk. 11:1-13

Yesu alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, “Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohane alivyowafundisha wanafunzi wake.” Akawaambia, “Msalipo, semeni, ‘Baba [yetu uliye mbinguni]. Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, [Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.] Utupe siku kwa siku riziki yetu. Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni [lakini tuokoe na yule mwovu].’”
Akawaambia, “Ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, ‘Rafiki yangu, nikopeshe mikate mitatu, kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake’; na yule wa ndani amjibu akisema, ‘Usinitaabishe; mlango umekwishafungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe’? Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake.

Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? au samaki, badala ya samaki atampa nyoka? au akimwomba yai, atampa nge? Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?”

TAFAKARI
TUMWOMBE YESU ATUFUNDISHE KUSALI: Wayahudi walikuwa watu wa sala. Walifundishwa na wazazi wao tangu wangali wadogo. Watoto wa kiume walifundishwa kusali kwa bidii sana kwa sababu, kadiri walivyotafsiri, sala ya Shema (Kum 6:4-9), dini ilikuwa ni amri na lazima kwa wanaume. Akina mama waliweza kusali au kwenda kwenye ibada sinagogini au hekaluni kwa hiyari yao tu. Pamoja na hayo, Mafarisayo au marabi waliwafundisha wanafunzi wao sala zao wenyewe. Ni katika kulifahamu hilo, wanafunzi wa Yesu walimwomba awafundishe kusali, naye akafanya mambo manne: alisali mwenyewe (Lk 2:42), aliwafundisha wengine kusali (Mt 6:5-13), aliainisha sifa nane za sala (Lk 11:5-14) na alielekeza namna ya kusali (Mt 6:5-6, Yn 14:13).
Sifa nane za sala waliweza kuzikusanya katika historia yao ya kumwangalia na kumsikiliza Yesu. Bila shaka walizing’amua sifa zifuatazo: kutumaini matashi ya Mungu kubariki, udumifu na uhakika, unyenyekevu, huruma, unyofu, msisitizo na uangalifu, muunganiko wa moyo na akili na hatimaye moyo wa kusubiri. Mintarafu namna ya kusali Yesu alisema watu wamwombe Mungu kupitia kwa jina lake huku akiacha uwezekano wa kumwomba kwa kupitia wengine (watakatifu) kabla ya maombi kufikishwa kwake.
Sifa ya kutumaini matashi ya Mungu kubariki imetambishwa kwa mifano. Mfano wa rafiki asiyechoka kumtafadhalisha rafiki yake aliyelala kitandani na wanawe. Wakati familia zililala pamoja na hata kujifunika shuka moja, mmoja alipoamka aliwarausha wote. Lakini kutokana na kudumu kwake katika kuomba msaada yule aliyekuwa amelala anakubali gharama za kuamka na kumpa mkate. Yesu anamaanisha Mungu hatakosa kututimizia maombi yetu ikiwa tunasali tukitumaini matashi ya Mungu kutubariki. Halafu Yesu anatoa mfano wa jinsi baba binadamu wanavyowajalia mambo mazuri watoto wao. Yesu anamaanisha Mungu hatasita kutujalia mema tumwombapo na bora zaidi kutujalia zawadi ya Roho Mtakatifu.
Somo la kwanza linatupa mfano wa sala nzuri ya Abrahamu aliyosali akiwaombea watu wa Sodoma na Gomora msamaha waachiliwe, hususan, wakiwapo watu wema kati yao. Alimwomba Mungu asiwe na hasira aseme naye kusudi hata wakionekana watu wema wachache kama kumi hivi watu wote wa Sodoma na Gomora waachiliwe. Mungu aliridhia ombi hilo, lakini kwa kuwa watu wema walikuwa pungufu mno Sodoma na Gomora hazikusalimika kibiriti cha moto. Somo hili linatuambia bayana kwamba tunaweza kuombeana na Mungu huwa tayari kutusaidia tunapoombewa. Kumbe, tuombeane.
Somo la pili linaonyesha kwa wazi faida ya kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua Yesu katika wafu. Somo linasema faida ni kufanywa hai pamoja na Kristo akiisha kutusamehe makosa yote baada ya kuwa tulikufa kwa sababu ya makosa yetu na kutokutahiriwa kwa mwili. Kifupi, tunaambiwa kutumaini matashi ya Mungu kubariki kuna faida isiyo na kipimo, siyo hapa duniani tu bali hata mwishoni mwa historia. Tusali kwa unyenyekevu na si kwa kumlazimisha. Kumbe, tusali kwa heshima, staha na taadhima; yeye atatutimizia tunachomwomba akiona yatufaa.

SALA: Ee Mungu mwema, wewe mwenyewe tufundishe kusali vyema. Tusisali ovyo tukikulazimisha msaada. Tunakuomba tunaposali vibaya na pasi heshima kwa ajili yetu au kwa ajili ya wengine, utusamehe. Amina.